Wakulima wa kijiji cha Isakamaliwa kitongoji cha Magogo wilaya Igunga Tabora wameilalamikia serikali ya wilaya hiyo kushindwa kutatua mgogoro wa ardhi kati yao na wafugaji wanaotoka katika maeneo ya wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, mgogoro ambao unafukuta kwa zaidi ya miaka miwili na kusababisha watu zaidi ya 200 kukimbilia kijiji jirani na kuishi maisha tegemezi.
Wakulima hao wapatao zaidi ya 200 wanaoishi nje ya makazi yao baada ya kufanyiwa vurugu na nyumba zao kuchomwa moto na watu wanaodhaniwa kuwa ni wafugaji wamepaza sauti zao na kuangua kilio mbele ya mkuu wa wilaya ya Igunga Bi. Zipora Pangani wakiiomba serikali kuingilia kati na kutatua mgogoro huo ili warudi katika maeneo yao na kuendelea na maisha ya kawaida.
Hali hiyo haikuathiri wakulima pekee bali hata vijana waliohitimu masomo ya elimu ya vyuo vikuu ambao walijikita katika kilimo cha mboga mboga nao wamejikuta wakiwa ni wahanga wa tukio hilo.
Licha ya serikali kutupiwa lawama kushindwa kutatua mgogoro huo uliodumu kwa muda mrefu mkuu wa wilaya ya Igunga Bi.Zipora Pangani ameeleza mikakati ambayo serikali imeamua kufanya ili kutatua mgogoro huo.
Tiba ya migogoro ya ardhi dhidi ya wakulima na wafugaji nchini bado haijapatikana huku hali hiyo ikionekana kuendelea kuzorotesha nguvu kazi ya Taifa.