Mgomo wa madereva wa daladala manispaa ya Morogoro umeingia siku ya pili baada ya madereva hao kuendelea kugoma wakishinikiza mamlaka ya udhibiti wa usafiri wa majini na nchi kavu (SUMATRA) mkoani humo kuyaachia magari yaliyokamatwa kwa makosa ya kutokuwa na leseni za usafirishaji abiria.
Akizungumza mbele ya mbunge wa jimbo la Morogoro mjini nje ya ofisi za Sumatra Mh, Abdula Ziz Abood katibu wa chama cha madereva Simoni Matiku amesema hawatasitisha mgomo huo hadi malalamiko yao ya msingi yatakapofanyiwa kazi.
Nao baadhi ya wamiliki wa daladala wamelalamikia Sumatra kuruhusu mabasi makubwa kuanza kusafirisha abiria ndani ya manispaa kinyume cha sheria huku mamlaka hiyo ikishindwa kutatua mgogoro wa madereva hao.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Morogoro Bwana Muhingo Rweyemamu ameagiza taratibu za upatikanaji wa leseni za magari yao zifanyike na magari yaanze kufanya kazi kauli inayopingana na msimamo wa mkurugenzi wa Sumatra makao makuu Bwana Giliadi Ngewe wakati akizungumza na Mutalemwa Blog kwa njia ya simu ambapo amesema Sumatra haitaachia magari hadi mahakama itakapotolea uamuzi.