Kituo cha afya cha Mwendakulima kinakabiliwa na upungufu wa dawa na vifaa tiba Shinyanga.
Kituo kipya cha afya cha Mwendakulima kilichoko wilayani Kahama katika mkoa wa Shinyanga kinakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa dawa, vifaatiba pamoja na uhaba wa wahudumu hali ambayo inasababisha wananchi wanaoishi katika kijiji hicho kufuata huduma za kiafya katika vituo vilivyoko katika vijiji vya jirani wakihofia kutopata huduma bora katika kituo hicho cha afya cha Mwendakulima.
Akizungumzia changamoto zinazokikabili kituo cha afya cha Mwendakulima ambacho kimejengwa kwa ufadhili wa kampuni ya ACACIA inayomiliki mgodi wa dhahabu wa Buzwagi muuguzi mfawidhi katika kituo hicho Bi.Selestina mbezi ameiomba serikali kupeleka wahudumu wa afya katika kituo hicho pamoja na kukipatia dawa na vifaa tiba vya kutosha ili kuokoa maisha ya wananchi wanaotumia muda mrefu kufuata huduma za kiafya katika vituo vingine vilivyoko mbali na kijiji hicho hali inayotishia kupoteza maisha ya wagonjwa hususan wanawake wajawazito.
Kwa upande wake afisa mtendaji wa kata ya Mwendakulima Bw.Mussa Ibingo amedai kuwa serikali inatambua mchango wa kampuni ya ACACIA katika kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo ya jamii hivyo kuna kila sababu za kuhakikisha serikali inapeleka dawa na vifaatiba vya kutosha katika kituo hicho mapema iwezekanavyo huku baadhi ya wagonjwa waliokuwa wakitibiwa katika kituo hicho cha afya wakionyesha kuridhishwa na kuduma waliyoipata.