Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye
amesema wanachama waliokihama chama hicho wamejivua nguo mbele za watu
na kwamba wapinzani wanaowachukua wanahangaika na mafuta machafu.
Aidha, amesema aliyekuwa Mbunge wa Segerea na Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk Milton Mahanga, alikuwa anatafuta sababu za kuihama CCM na anamtakia kila la heri, yeye na rafiki yake, Edward Lowassa.
Nape aliyasema hayo jana katika mkutano
wake na waandishi wa habari katika Ofisi Ndogo ya CCM Lumumba, Dar es
Salaam, alipotakiwa kueleza kuhusu kuhama kwa Lowassa na Dk Mahanga
ambao wote kwa nyakati tofauti wamekimbilia Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA).
Lowassa alijitoa CCM wiki moja iliyopita
baada ya kukwama uteuzi wa CCM wa kuwa mgombea wake wa urais na
kukimbilia Chadema ambako anatarajiwa kuwa mgombea wake wa urais na
kuungwa mkono na Umoja wa Vyama vinne vya Upinzani (UKAWA).
Dk Mahanga naye alijitoa juzi baada ya
kukwama katika kura za maoni jimboni Segerea. “Wanahangaika na oil
chafu. Hawa ni wale wale kama ilivyokuwa Mrema (Augustino) mwaka 1995,
akabebwa kiasi cha Mwalimu Nyerere kusema mwacheni abebwa.
Hebu jiulizeni wanaona ubaya wanapotoka,
lakini mambo yakiwanyookea hawasemi, wakitoka ndio maneno mengi,”
alisema Nape. Alisema kuondoka kwa Lowassa na wengine wachache, si jambo
la kwanza kutokea CCM, na pia si la ajabu wala haliwezi kuwa la mwisho
huku akimtuhumu Dk Mahanga kuwa alikuwa akitafuta sababu ya kuondoka
CCM.