Jumla ya Shl. Milioni 370 za kitanzania, zinahitajika kwa ajili ya Ukarabati wa Jengo la Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi ulipo Wete Kisiwani Pemba.
Kupatikana kwa Pesa hizo kutaiwezesha Serikali kuweka Samani na Vifaa vya kisasa kwa ajili ya kuendeleza Shughuli za Baraza la Wawakilishi Kisiwani Pemba kama ilivyokuwa mwanzoni.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mohamed Aboud wakati akijibu Swali la Mwakilishi wa Jimbo la Wawi Saleh Nassor Juma katika Kikao cha Bajeti kinachoendelea Chukwani nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Amesema miaka ya nyuma kulikuwa na utaratibu wa kufanyika Vikao vya Baraza la Wawakilishi kwa mpangilio maalum baina ya Kisiwa cha Unguja na Pemba lakini kwa sasa utaratibu huo umeondoka.
Amesema kukosekana kwa Vikao vya Baraza la Wawakilishi Pemba kumetokana na Ukumbi wa Baraza hilo uliopo Pemba kukosa Viwango vinavyohitajika.
Hata hivyo Waziri Aboud amesema nchi nyingi Duniani Vikao vya Baraza au Bunge huwa vinafanyika pahala pamoja tu jambo ambalo ni tofauti na Zanzibar.
Amesema licha ya tofauti hiyo bado Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaona ni vyema kuendeleza utamaduni wa kufanya Vikao vyake Unguja na Pemba hasa pale Ukumbi huo Utakapomaliza matengenezo yake.