Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu Mhe. Bahame Nyanduga akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa ya uchunguzi wa tuhuma dhidi ya Jeshi la Polisi za kuwapiga na kuwazalilisha Viongozi na Wafuasi wa CUF huko Mtoni Mtongani Temeke, Dar es sa Salaam.
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imelaani vitendo vya uzalilishaji vilivyofanywa kwa Viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) Januari 27 mwaka huu (2015) wakati wa maandamano ya Chama hicho Mtoni Mtongani Wilaya ya Temeke.
Akizungumza na waandishi wa habari jana (Mei 20, 2015) Jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Bahame Nanduga, alisema uchunguzi wa tukio hilo umekamilika kwa kuzingatia kifungu cha 130[1][c],[f] na [g] cha katiba ya jamhuri ya Tanzania.
Aidha aliongeza kuwa sheria nyingine zilizotumika kuchunguza tukio hilo ni pamoja na kifungu cha 6[1][c]na [g] vifungu 15[1][a] na 28[1][a],[b] na f vya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Na.7 ya mwaka 2001, sheria ya polisi na polisi wasaidizi, sura 322, na sheria ya vyama vya siasa, sura 258
Nyanduga alisema Tume yake imebaini ukikwaji mkubwa wa haki za binadamu waliofanyiwa viongozi na wanachama chama cha wananchi CUF katika maandamano yao ya shughuli za kichama, hivyo Tume ilibaini kuwa jeshi la polisi lilitumia nguvu kupita kiasi, ukiukwaji wa misingi ya utawala bora na udhalilishaji wa wanachama wawili wa kike wa CUF.
“Tume imetoa mapendekezo kwa jeshi la polisi kuzingatia kanuni, sheria, haki za binadamu na misingi ya utawala bora katika utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku na kuhakikisha maafisa wake wanajipanga vyema katika kuratibu na kusimamia utekelezaji wa operesheni zake” alisema Nyanduga
Kwa mujibu wa Nyanduga tume hiyo pia imewataka Viongozi na wanachama wa CUF kutafuta namna ya kuboresha mahusiano na jeshi la polisi, ili kuondoa mivutano isiyo na tija.
Tume imepanga kuitisha mafunzo na mikutano mbalimbali kwa kushirikiana na vyama vya siasa,Tume ya Taifa ya Uchaguzi [NEC], pamoja na vyombo vya Ulinzi na Usalama ikiwemo Jeshi la Polisi na Magereza, msajili wa vyama vya siasa, na asasi za kiraia ili kupanga taratibu zote katika kujua haki za binadamu na utawala bora.