Takriban magari milioni thelathini na nne 34,000,000 yanatarajiwa kurejeshwa viwandani nchini Marekani kufuatia hitilafu ya kiufundi kwenye mifuko ya hewa ya usalama.
Kampuni inayotengeneza mifuko ya hewa ya usalama ya magari inachukua hatua hiyo baada ya malalamiko kuwa hitilafu ya muundo wake imesababisha vifo vya watu wapatao watano.
Tukio hili la urejeshwaji wa magari viwandani kutokana na kasoro za kiufundi ni kubwa zaidi kuwahi kutokea nchini Marekani. Kampuni ya kutengeneza vifaa vya magari ya Japan, Takata, imekiri mifuko ya hewa kulinda usalama wa watumiaji wa magari kuwa na kasoro.
Baadhi ya mifuko hiyo ya hewa imepasuka kwa nguvu kupita kiasi na kusababisha kurusha vipande vya chuma kwa madereva na abiria wanaokaa viti vya mbele.
Waziri wa Usafirishaji wa Marekani, Anthony Foxx, ametangaza kurejeshwa kwa magari yenye hitilafu ya mfumo huo kote nchini humo.
Bwana Foxx amesema urejeshwaji wa magari hayo ni kazi kubwa.
Tangazo hilo limetolewa na Utawala wa usalama wa taifa nchini Marekani katika barabara Kuu baada ya mazungumzo marefu na kampuni ya Takata.
Magari yanayorejeshwa yanahusu kampuni kumi na moja za kutengeneza magari zikiwemo za Honda, Toyota na Nissan.
Urejeshwaji viwandani kwa magari mapya hufanyika baada ya kugundulika hitilafu lolote la kiufundi linaloweza kuhatarisha usalama wa watumiaji wa magari hayo.