WIZARA YA AFYA NA USTAWI WA JAMII
TAARIFA KWA UMMA KUHUSU UGONJWA WA HOMA YA DENGUE “DENGUE FEVER”
Utangulizi
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inapenda kutoa taarifa kwa umma juu ya kuwepo kwa ugonjwa wa homa ya dengue yaani “dengue fever” hapa nchini. Ugonjwa huu umethibitishwa baada ya sampuli zilizochukuliwa kutoka kwa watu waliohisiwa kuwa na ugonjwa huu jijini Dar es salaam kupelekwa kwenye maabara yetu ya Taifa Dar es salaam na kuthibitisha kuwa na virusi vya homa ya dengue mnamo mwishoni mwa mwezi wa Januari. Hadi sasa idadi ya wagonjwa ambao wamethibitishwa kuwa na ugonjwa huu ni
21 na hakuna mgonjwa yeyote aliyepoteza maisha.
Homa ya Dengue
Homa ya dengue ni ugonjwa unaosababishwa na kirusi ambacho kinaenezwa na mbu wa aina ya Aedes.
Dalili za ugonjwa huu ni homa, kuumwa kichwa, maumivu ya viungo na uchovu. Dalili hizi huanza kujitokeza kuanzia kati siku ya 3 na 14 tangu mtu alipoambukizwa kirusi cha homa ya dengue. Wakati mwingine dalili za ugonjwa huu zinaweza kufanana sana na dalili za malaria, hivyo basi wananchi wanaombwa kuwa wakati wakipata homa kuhakikisha wanapima ili kugundua kama wana vimelea vya malaria ua la ili hatua stahiki zichukuliwe.
Virusi vya homa ya dengue vinaenezwa kwa binadamu baada ya kuumwa na mbu aina ya “Aedes”. Mbu hawa hupendelea kuzaliana kwenye maji yaliyotuama karibu na makazi ya watu au hata ndani ya nyumba. Viluwiluwi vya mbu hawa huweza kuishi katika mazingara ya ndani ya nyumba mpaka wakawa mbu kamili na kuanza kusambaza ugonjwa huu kwa binadamu. Mbu hawa huwa na tabia ya kuuma wakati wa mchana.
Ugonjwa huu hauenezwi kutoka kwa binadamu mmoja kwenda kwa mwingine. Homa ya dengue inaweza kutibika kama mgonjwa atapelekwa hospitali mapema na kupatiwa matibabu ya haraka. Hakuna tiba maalumu ya ugonjwa wala chanjo bali mgonjwa anatibiwa kutokana na dalili zitakazoambatana na ugonjwa huu kama vile homa, kupungukiwa maji au damu. Endapo mgonjwa atachelewa kupatiwa matibabu, mgonjwa anaweza kupoteza maisha.
Jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa homa ya dengue
Kuangamiza mazalio ya mbu
- Fukia madimbwi ya maji yaliyotuama au nyunyuzia dawa ya kuua viluwiluwi vya mbu kwenye madimbwi hayo
- Ondoa vitu vyote vinavyoweza kuweka mazalio ya mbu kama vile, vifuu vya nazi, makopo, magurudumu ya magari yaliyotupwa hovyo, nk.
- Fyeka vichaka vilivyo karibu na makazi ya watu
- Hakikisha maua yandayopandwa kwenye makopo au ndoo hayaruhusu maji kutuama
- Funika mashimo ya maji taka kwa mfuniko imara
- Safisha gata za paa la nyumba ili kutoruhusu maji kutuama
Kujikinga na kuumwa na mbu
- Kumia dawa za kufukuza mbu “mosquito repellants”
- Vaa nguo ndefu kujikinga na kuumwa na mbu
- Tumia vyandarua vyenye viuatilifu (hata kwa wale wanaolala majira ya mchana)
-Weka nyavu kwenye madirisha na milango ya nyumba za kuishi
Hatua zinazochukuliwa na Wizara
•Kutoa taarifa ya tahadhari ya ugonjwa kwa Waganga Wakuu wote wa Mikoa na Wilaya kwa Tanzania Bara kupitia Makatibu Tawala na Wakurugenzi.
•Kuimarisha ufuatiliaji wa ugonjwa huu kupitia kwa Wataalamu wa Afya katika Mikoa, Wilaya na maeneo ya mipakani. Aidha uchunguzi wa ugonjwa huu utafanyika kwenye Mikoa na Wilaya zitakazoonekana kuwa na ongezeko la wagonjwa wenye homa.
•Kutuma vipeperushi vya ugonjwa huu katika maeneo ya mipakani ili iwapo msafiri anayeondoka au kurudi nchini akiwa na dalili tajwa atoe taarifa kwa watumishi wa afya wa mpakani ili hatua stahili ziweze kuchukuliwa.
•Kutoa mafunzo kwa watumishi wa afya na mipakani wa namna ya kutambua na kujikinga dhidi ya maambukizo ya ugonjwa huu pamoja na uchukuaji wa sampuli iwapo mgonjwa atapatikana.
•Kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa nchi nzima kwa kutumia mfumo uliopo wa ukusanyaji wa taarifa, ambapo tunaendelea kupata taarifa za kila siku juu ya mwenendo wa ugonjwa huu
•Kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji wa ugonjwa wa dengue uliopo kwenye vituo maalumu ‘Sentinel Surveillance Sites’
•Kuimarisha Utambuzi wa ugonjwa katika maabara ili kuweza kuthibitisha ugonjwa huu
•Kufanya tathmini ya mazalio ya mbu ili kubaini ukubwa wa tatizo, jamii ya mbu wanaoambukiza ugonjwa, mazingira yao na jinsi ya kuwathibiti
Hitimisho
Wananchi wanashauriwa kutokuwa na hofu kuhusu ugonjwa huu bali wanashauriwa kwenda katika vituo vya tiba mara mnapoona dalili.
Ugonjwa huu si mpya.
Mara ya kwanza kugundulika kuwepo kwa ugonjwa huu nchini ilikuwa ni Juni 2010 mkoani Dar es salaam ambapo idadi ya watu waliothibika kuwa na ugonjwa ilikuwa 40, pia kati ya mwezi Mei hadi Julai 2013, wagonjwa 172 walithibitishwa kuwa na ugonjwa huu. Hakuna mgonjwa yeyote aliyepoteza maisha.
Wizara inasisitiza kuwa hakuna vikwazo vyovyote vilivyowekwa kwa ajili ya wasafiri wanaoingia na wanaotoka nchini. Wizara itaendelea kushirikiana na sekta mbalimbali kufuatilia na kudhibiti ugonjwa huu.
Angalia video hapo chini inayo onesha jinsi ugonjwa unavyo sambaa.
Kwa habari za Matukio Kitaifa, Kimataifa, Michezo na Burudani, Ungana nami kupitia Link zifuatazo.