Mwanamke mmoja na watoto wake wawili, wameokolewa na wasamaria wema baada ya kufungiwa na mumewe kwenye nyumba bila huduma muhimu kwa miaka mitatu mfululizo kwa sababu ya wivu.
Tukio hilo limetokea kijiji cha Longuo wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro. Mwanamke huyo, Janeth Barama kutoka kijiji cha Ilula mkoani Iringa, alisema mumewe Arcado Massawe ni mlevi wa gongo na bangi. Alisema kipindi chote walichokuwa kifungoni walikuwa wakijisaidia ndani huku akiwaletea chakula kidogo mara chache kwa wiki.
Alidai kuwa sababu ya kufungiwa ndani ni wivu wa kimapenzi kwa hofu kuwa atafanya mapenzi na wanaume wengine. Huku akibubujikwa na machozi, alisema mume wake huondoka kila siku saa 11 alfajiri na kurudi saa 9 usiku akiwa amelewa chakari na humpiga bila sababu. Aliomba serikali imchukulie hatua kali mumewe kwa kuwa akiachiwa anaweza kuwaua.
Alisema mume wake anafanya kazi ya ulinzi katika nyumba hiyo ambayo mmiliki wake anaishi jijini Dar es Salaam. Hata hivyo, alisema bosi wa mumewe hana taarifa za vitendo vya kinyama anavyofanyiwa na mfanyakazi wake.
Aliendelea kusimulia kuwa mtoto wake wa pili, Zuena Massawe (1.2), alijifungua akiwa amefungiwa ndani ya nyumba hiyo na kwa muda wote uzazi wake hakuwahi kupelekwa kliniki lakini anamshukuru Mungu mtoto yuko salama.
Watoto hao, Zuena na kaka yake, Obama Massawe (3.5), wameathirika kiafya kutokana na kuwa na utapiamlo. Alisema hii ni mara ya pili kwa mumewe kumfungia kwenye nyumba kwani mara ya kwanza wakati anafanya kazi kwa bosi mwingine alimfungia kwa miezi sita na bosi alipogundua alimfukuza kazi.
Mwenyekiti wa kijiji hicho, Gerson Mambo alisema, jana ndiyo waligundua kuwa ndani ya nyumba hiyo wanaishi binadamu baada ya mwanamke huyo kupiga mayowe ya kuomba msaada. Alisema alitoa taarifa kwa afisa mtendaji wa kijiji ambaye alipiga simu polisi na kuvunja mlango.
Baadhi ya majirani wameviomba vyombo vya dola vimsaidie mwanamke huyo apate haki zake za kimsingi na watoto wake na kumrejesha kijijini Ilula kwa wazazi wake.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu, Kamanda wa polisi mkoani Kilimanjaro, Robert Boaz alisema, mtuhumiwa ametiwa mbaroni na anatarajiwa kufikishwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.
Aliwapongeza wananchi kwa kutoa taarifa kituo cha polisi na kumwokoa mwanamke huyo ambaye angeweza kupoteza maisha na watoto wake.
Jiunge na mi kwa kubonyeza kwenye link zifuatazo chini ili kupata habari mpya zaidi.
FACEBOOK >>> TWITTER >>> MATUKIO KWA NJIA YA SAUTI