SIKU moja baada ya Rais Jakaya Kikwete kuwataka viongozi wa dini kuombea wajumbe wa vyama vya siasa vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) – CCM, CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi - kwa maelezo kuwa ndio waliochafua hali ya hewa na kukwamisha mchakato wa Katiba Mpya, viongozi hao wamejibu mapigo wakisema yeye ndiye amelikoroga, hivyo lazima alinywe.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti la hili, walisema Rais Kikwete ndiye mtuhumiwa namba moja wa kuvuga mchakato wa kuandikwa kwa katiba mpya.
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, alisema Rais Kikwete alipaswa kuwaambia viongozi wa dini wamwombee yeye kwa kuwa kundi la UKAWA liliundwa kwa sababu yake.
“Natumia lugha kali na ninarudia kusema kuwa Rais Kikwete ndiye anayepaswa kuombewa mapepo kwa sababu anachanganya kauli bila kuelewa nafasi aliyonayo katika mchakato huu tangu alipouanzisha,” alisema Dk. Slaa
Dk. Slaa alisema Rais Kikwete aliamua makusudi kuvuruga Watanzania kwa kusisitiza msimamo wake na chama chake uwe ndio msimamo wa wananchi, kinyume cha Rasimu ya iliyowasilishwa na Jaji Joseph Warioba, ambayo imesainiwa na rais mwenyewe.
“UKAWA haitaachia msimamo wake mpaka hapo Rais Kikwete atakapokiri kwa maandishi kuwa ndiye aliyewavuruga, hivyo waandelee na mchakato. Mapepo yako kwake si kwa wana-UKAWA,” alisema.
Naye Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe alisema chama chake kinaamini kwamba aliyeharibu mchakato wa katiba mpya ni Rais Kikwete na wajumbe wa Bunge la katiba kutoka CCM.
Akifafanua kauli yake, Nyambabe alisema maoni aliyoyatoa Rais Kikwete alipozindua Bunge hilo ndiyo yamesababisha mvurugano uliopo kwa kuwa kilichoendelea baada ya hapo ni kujadili maoni yake badala ya kujadili rasimu ya katiba.
“Nafikiri Rais Kikwete akiri kwamba amewakoroga watanzania katika suala hili la katiba, alitakiwa kuwaomba viongozi wa dini wamwombee yeye na sio sisi ambao tunapigania maoni ya wananchi yaliyomo kwenye rasimu,”alisema
Naibu Mkurugenzi wa Habari wa Chama cha Wananchi (CUF), Abdul Kambaya alisema kuwa; “Rais anaposema kuhusu uwepo wa mapepo anatakiwa kufahamu kuwa yeye ndiye aliyeyasafirisha kuingia bungeni kupitia taasisi yake, manaa kabla ya hapo kulikuwa na mariadhino tu na mambo yalikuwa yakienda vizuri,”alisema.
Nako mkoani Mbeya, wananchi wamembana Rais Kikwete wakisema ndiye anapaswa kuombewa kwanza kwa vile aliasisi mchakato huo na kisha kuuvuruga alipozindua Bunge la Katiba.
Ikulu yakwepa UKAWA
Wakati huo huo, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, amesema kuwa dhamira ya wajumbe wa kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ya kutaka kukutana na Rais Jakaya Kikwete kujadili hali tete ya kukwama kwa mchakato wa Katiba mpya, haiwezi kuwa na miujiza yoyote kama vyama vya siasa havitakuwa na muafaka kabla ya kufika Ikulu.
Akizungumza na gazeti hili kwa simu jana, kuhusu sharti hilo la UKAWA, Balozi Sefue alisema badala ya viongozi hao kufikiria kwenda Ikulu ni vema wakatumia mabaraza ya mashauriano kutafuta suluhu ya mambo wanayotofautiana kwa ajili ya mustakabali wa Taifa.
Balozi Sefue aliainisha kuwa Rais Kikwete hana mamlaka ya kuingilia kanuni zinazoongoza Bunge Maalum la Katiba.
Licha ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi na Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta, kuendesha jitihada za kutafuta maridhiano, UKAWA wamepinga vikao hivyo wakidai viongozi hao hawana uamuzi na hivyo kutaka wakutane na Rais Kikwete mwenyewe kwa sababu ndiye alivuruga mchakato huo wakati wa uzinduzi wa Bunge Maalum.
Alipoulizwa Balozi Sefue kama Ikulu iko tayari kuridhia sharti la UKAWA, alisema nia ya Rais Kikwete siku zote ni kuona mchakato wa katiba unamalizika kwa wakati na kwa amani na kwamba Ikulu haiwezi kuingilia kanuni za Bunge zilizokubaliwa kutumiwa kama muongozo na wajumbe hao.
“Wao wanataka kukutana na Rais, ninachojua hayo wanayoyasema yapo katika miongozo yao ya Bunge kwa kuwa limeanzishwa kwa mujibu wa sheria na walikubaliana namna watakavyofanya kazi ya kupata katiba mpya,”alisema Sefue.
Alipoelezwa kuwa mwenye uwezo wa kuamua juu ya hatma ya mchakato wa katiba pamoja na Bunge lake kwa sasa ni Rais Kikwete kutokana na msimamo wake aliouonyesha wakati kulizindua kwa kukataa muundo wa serikali tatu uliopendekezwa na rasimu, alisema hana hakika kama ni sahihi kwa rasimu hiyo kujadiliwa kama ilivyo.
“Pengine ni muhimu uongee na mwanasheria mkuu wa serikali, yeye anaweza kutoa ufafanuzi kama ni jambo la busara rasimu ijadiliwe kama ilivyo au kama Bunge halina mamlaka ya kubadilisha baadhi ya vitu,”alisisitiza.
Jiunge na mi kwa kubonyeza kwenye link zifuatazo chini ili kupata habari mpya zaidi.