Katibu Mkuu wa shirikisho la mpira wa miguu nchini (TFF) Selestine Mwesigwa amesisitiza umuhimu wa programu za vijana kwa maendeleo ya soka nchini na kuitaka kampuni ya simu za mkononi ya Airtel Tanzania kuangalia uwezekano wa kuwa wadhamini wa timu ya Taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20.
Baadhi ya washiriki wa semina elekezi ya Airtel Rising Stars wakifutilia kwa makini moja ya mada zilizowasilishwa kwenye semina hiyo iliyofanyika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
Akifungua semina elekezi kwa makatibu wakuu wa mikoa inayoshiriki mashindano ya vijana ya Airtel Rising Stars (ARS) iliyofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Jumamosi Julai 19, 2014 Mwesigwa alisema hali halisi inaonyesha kwamba miaka michache ijayo wachezaji wengi watakaounda timu ya taifa ya U-20 watatokana na ARS hivyo ni vema kampuni ya Airtel ikawa mdhamini mkuu wa timu hiyo.
Meneja Matukio wa Airtel Tanzania Rebeca Mauma akizungumza wakati wa semina elekezi ya Airtel Rising Stars iliyofanyika kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
Alisema kuwa suala la programu za vijana ni agenda namba moja ya TFF na kuzitaka timu za ligi kuu kuzingatia maagizo ya shirikisho hilo la kuwa na timu za vijana. “Klabu ya Simba imefanikiwa sana katika suala hili na ni vema timu nyingine za ligi kuu zikaiga mfano huo”, alisema Mwesigwa na kuipongeza Airtel kwa kuwekeza katika soka la vijana.
“Wachezaji wanapolelewa na klabu tangu wakiwa wadogo inakuwa ni rahisi kwao kuendana na maadili ya klabu hiyvo kuwa na wachezaji wenye nidhamu ya hali ya juu tofauti na wachezaji waosajiliwa kutoka sehemu mbali mbali wakiwa na umri mkubwa”, alisema.
Aliwataka makatibu hao wa mikoa kuzingatia kanuni ikiwa ni pamoja na umri ili kuwafanya vijana watakaoshiriki mashindano ya Airtel Rising Stars kuwa na ushindani ulio sawa. Mashindano ya ARS yanashirikisha vijana chini ya umri wa miaka 17.
Katibu mkuu wa TFF Selestine Mwesigwa akisisitiza jambo wakati wa semina elekezi ya Airtel Rising Stars iliyofanyika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
Mwesigwa aliungwa mkono na Mwenyekiti wa kamati ya vijana ya TFF Ayoub Nyenzi aliyesema kuwa programu za vijana e.g. ARS ndiyo mkombozi wa kweli wa soka popete pale duniani.
Mashindano hayo yanatarajiwa kuanza kutimua vumbi katika ngazi ya mkoa Julai 27 na kushirikisha mikoa ya Mbeya, Morogoro, Mwanza, Ilala, Kinondoni na Temeke kwa upande wa wavulana huku timu za wasichana zikitoka mikoa ya Mwanza, Mbeya, Zanzibar, Ilala, Kinondoni na Temeke.
Akiongea katika semina hiyo Meneja Uhusiano wa Airtel Tanzania Jackson Mmbando aliwapongeza viongozi wa mikoa kwa kazi nzuri iliyoiwezesha Tanzania kutwaa ubingwa wa mashindano ya kimataifa ya ARS (wasichana) yaliyofanyika Nigeria na kuzawadiwa USD 10,000, medali na vikombe.
“Vile vile timu ya wavulana ilifanya vizuri sana na ni imani yangu kwamba mwaka huu Tanzania itashinda vikombe kwa wasichana na wavulana”, alisema na kusisitiza nia thabiti ya Airtel kuendelea kuboresha mashindano hayo.
Naye Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF Salum Madadi aliwataka makatibu hao kufanyakazi kwa karibu na kamati ya vijana ya TFF inayosimamia mashindano hayo.
Meneja Uhusiano wa Airtel Tanzania Jackson Mmbando akiteta na Katibu Mkuu wa TFF Selestine Mwesigwa wakati wa semina elekezi ya Airtel Rising Stars iliyofanyika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. Kushoto ni Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF Salum Madadi na Mwenyekiti wa DRFA Almasi Kasongo.
Jiunge na mi kwa kubonyeza kwenye link zifuatazo chini ili kupata habari mpya zaidi.