SERIKALI imepongezwa kwa kutambua juhudi zinazofanywa na wasanii, wanamichezo na waandishi wa habari za kujenga nyumba za makazi katika kijiji cha Mwanzega Mkuranga ambapo Mwenge wa Uhuru ulifika na kuweka jiwe la msingi Julai 22 mwaka huu.
Mwenyekiti wa Mtandao wa Wasanii Tanzania (SHIWATA),Cassim Taalib katika risala aliyosoma mbele ya Kiongozi wa Mwenge kitaifa, Rachael Kassanda alisema Serikali kukitambua kijiji hicho kumeongeza ari ya wasanii kujenga nyumba za kisasa na kuongeza kasi ya maendeleo.
Alisema kijiji cha wasanii kimeanzishwa mahususi kwa ajili ya kuwakomboa na kuwapatia makazi ya kudumu wakisha staafu au kupotea kwa umaarufu wao katika fani zao.
Katika sherehe hizo ambazo wasanii zaidi ya 1,500 waliofurika kupokea mwenge wa uhuru kiongozi wa mbio za Mwenge, Rachael Kassanda aliwatoa wito kwa wasanii kuwa kioo halisi cha jamii kwa kuiga mema na kupiga vita mabaya katika jamii zinazowazunguka.
Awali Mkuu wa wilaya ya Mkuranga, Mercy Sila aliwaasa wasanii kutumia vipaji vyao kuwaelimisha jamii kuhusu maadili mema na kuiga yanayostahili kwa mila na desturi za Mtanzania.
Katika sherehe za kuweka jiwe la msingi zilizofanywa na kiongozi wa mbio za Mwenge,SHIWATA ilimsimika balozi wa kijiji hicho kuwa ni msanii maarufu na mtangazaji wa kituo cha Redio Times FM, Suzan Natasha ambaye aliahidi kukitangaza kijiji hicho katika mipaka ya ndani na nje ya Tanzania.
Sherehe hizo zilizoambatana na burudani mbalimbali zilizongozwa na Bendi ya Polisi, wanamuziki maarufu Kikumbi Mwanzo "King Kikii", Siza Mazongera "Wana Segere" na wasanii mbalimbali walitumbuiza.
Wengine walioshudia kuwekwa jiwe la msingi katika kijiji hicho baadhi yao ni wachezaji wa zamani wa Simba, Moses Mkandawile, George Lucas,Thom Kipese na kwa upande wa Yanga ni Abeid Mziba, Ramadhani Kampira, Bakari Malima, Omari Husein na wengineo.
Pia katika kusherekea mwenge wa uhuru SHIWATA ilitoa ofa bure kwa wanachama wapya kupimiwa viwanja vya kujenga nyumba bure katika kijiji hicho ambapo wanamichezo, wasanii na waandishi wa habari walipata fursa ya kuoneshwa viwanja watakavyotakiwa kujenga.
Jiunge na mi kwa kubonyeza kwenye link zifuatazo chini ili kupata habari mpya zaidi.