Zaidi ya walimu 100 wanaofundisha shule mbalimbali wilayani Igunga, wamefunga Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Igunga wakishinikiza kulipwa mishahara yao na posho wanazodai.
Hatua hiyo ilisababisha watumishi wa halmashauri hiyo kukaa nje ya ofisi, hali iliyosababisha wananchi kukosa huduma kwa zaidi ya saa nne. Wakizungumza kwa nyakati tofauti juzi, walimu hao wakiwa wameweka uzio kwenye ofisi ya mkurugenzi, walisema wanasikitishwa na kitendo cha kucheleweshewa mshahara wa mwezi Aprili na malimbikizo ya posho zao.
Walisema kukosa mshahara na posho zao imesababisha kuishi maisha magumu kwenye vituo vyao vya kazi. Walidai tangu waripoti wilayani Igunga wamekuwa wakifuatilia mishahara yao na posho bila mafanikio, huku wakitumia nauli ambazo hawarudishiwi.
Kuhusu kufunga ofisi hizo, walimu hao walisema wamechukua uamuzi huo ili kumpa salamu mkurugenzi kwamba wanaishi maisha ya shida. “Tunasikitika mishahara na posho ni haki yetu, kwani maisha tunayoishi vijijini ni magumu sana hivyo leo hatuondoki mpaka tutakapolipwa mishahara na posho zetu,” alisema mmoja wa walimu hao.
Polisi wakiwa na zana zote za kupambana iwapo fujo zingetokea, ila walimu walikuwa watulivu. Akizungumza na walimu hao, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Rustica Turuka alisema mishahara haijapelekwa kutoka Hazina na kuwaomba walimu kuwa na subira.
“Ndugu zangu walimu sina lengo baya na ninyi, kwani hizo fedha ni mali yenu lakini tatizo lipo Hazina hadi sasa tunavyozungumza mishahara yenu haijaletwa kwenye halmashauri yangu,” alisema Turuka.
Turuka alisema wamejipanga kutafuta angalau Shilling 44 milioni kuwakopesha walimu hao, ili kuwasaidia wakisubiri mishahara ambayo hakutaja kiwango chake cha posho zao.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Igunga, Alphonce Kasanyi aliwaomba walimu hao kuendelea kuvuta subira wakati Serikali ikishughulikia mishahara yao. Hata hivyo, hadi majira ya mchana walimu walikuwa wamefungua ofisi ya mkurugenzi huyo.