CHONDE chonde waamuzi miliopangwa kuchezesha mechi za leo za ligi kuu soka Tanzania bara ambazo zinahusisha timu mbili za Yanga na Azam fc zilizopo katika kinyang`anyiro cha kuwania ubingwa.
Yanga wanacheza dhidi ya Kagera Sugar ndani ya uwanja wa Taifa, wakati Azam fc wanacheza na Ruvu Shooting katika uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.
Ukubwa wa mechi hizi haujengwi katika misingi ya majina ya timu pinzani kwa timu hizi mbili zilizopo nafasi mbili za juu.
Yanga kwa jinsi walivyo na ukongwe wao huwezi kuwafananisha hata kidogo na Kagera Sugar.
Kagera wamezidiwa karibu kila kitu na Yanga, hivyo mechi hii haina msisimko kwa kuangalia majina ya timu hizi mbili.
Ingekuwa Simba dhidi ya Yanga, hapa majina na ukongwe karibia unafanana kwa kila kitu, na kwa maana hiyo, `presha` ya mchezo huanza kwenye majina kwanza.
Mtu akisikia Simba na Yanga zinapambana, lazima ahamasike na kutaka kujua nini kitatokea.
Pia kwa Azam fc na Ruvu Shooting kuna utofauti wa majina. Wana Lambalamba hawana ukongwe wowote wa ligi kuu Tanzania bara, lakini mipango yao, jitihada zao na uwezekezaji mkubwa walioweka katika timu yao, kumeifanya klabu hii iwe na mvuto kwa mashabiki wa soka.
Kwa maana hiyo, Azam fc ni timu kubwa kuliko Ruvu Shooting na kila mtu atafuatilia mchezo huu kutaka kujua nini Azam fc watapata huko Mabatini.
Kama ushindani wa mechi za leo hauangaliwi kwa majina ya timu zinazocheza kwasababu hazilingani hata kidogo, je, nini kinazifanya mechi hizi kuwa na `Presha` kubwa?.
Jibu ni rahisi tu. Matokeo yanayohitajika ndio sababu ya msingi ya mechi hizi kuwa ngumu zaidi leo hii.
Yanga wanahitaji pointi tatu muhimu, na mashabiki wake lukuki waliopo nyuma wanahitaji kuona timu yao inashinda.
Mpaka sasa Yanga wapo nafasi ya pili katika msimamo baada ya kucheza mechi 23 na kujikusanyia pointi 49.
Ili kueteta ubingwa wao, wanahitaji kushinda mechi zote tatu zilizosalia huku wakiwaombea mabaya Azam fc waliopo kileleni kwa pointi pointi 53 baada ya kucheza mechi 23.
Kwa mazingira hayo, Yanga kwa namna yoyote ile matokeo mazuri kwao ni ushindi tu.
Sare au kufungwa itakuwa mwiba mkubwa kwao, kwasababu hawana uhakika wa nini kitamtokeo Azam fc.
Hali kadhalika, Azam fc wanahitaji matokea kwa nguvu zote ili kuzidi kukaa kileleni.
Azam wanahitaji ushindi wa mechi mbili tu kati ya tatu zilizosalia ili kujitangazia ubingwa wao wa kwanza tangu wapandae msimu wa 2008/2009.
Hii ni mechi ngumu kwao ukizingatia wapo uwanja wa mabatini ambao Ruvu Shooting wamekuwa wagumu kufungwa.
Kutokana na mazingira haya, michezo hii miwili imevuta hisia za mashabiki wengi.
Inafahamika kuwa Ruvu Shooting na Kagera Sugar si washindani wa nafasi tatu za juu, lakini watahitaji kuandika historia ya kuzisumbua timu mbili zinazowania ubingwa.
Azam fc hawajawahi kufungwa katika michezo 23 waliyocheza msimu huu, labda Ruvu Shooting wanaweza kuwa wa kwanza kuwatibulia rekodi yao.
Kama mechi zipo katika mazingira haya, cha kuandika kuhusu upande wa pili wa mchezo na watatu kwa maana ya waamuzi na mashabiki kinapatikana.
Waamuzi wa leo wajue fika kuwa wanachezesha mechi ambazo timu zinahitaji matokeoa kwa njia yoyoye.
Hivyo lazima sheria 17 zinazoendesha mpira wa miguu zifuatwe kwa umakini mkubwa.
Nafahamu yapo makosa ya kibinadamu kwa waamuzi, lakini kama watafanya makosa kwa shinikizo la mazingira fulani, wataathiri ubora mechi hizo.
Kinachotakiwa kwa waamuzi ni kusimamia sheria 17 na kuwaza mara mbili mbili wanapotoa maamuzi.
Wanatakiwa kukwepa maamuzi tata uwanjani kwani `presha` ya mechi ni kubwa sana kuanzia kwa mashabiki, mabenchi ya ufundi na wachezaji wenyewe.
Moja ya sababu inayowafanya waamuzi kushindwa kumudu baadhi ya mechi ni `presha` ya mechi zenyewe.
Ni kazi ngumu kuchezesha mechi ya Simba na Yanga kwani ukikosea tu unaonekana kama unaipendelea timu fulani.
Kuna wakati mwamuzi lazima ujenge mazingira ya kuaminiwa. Fanya maamuzi sahihi na kwa mawasiliano na wenzako.
Wapo wasaidizi wa mwamuzi wa kati, hivyo ni kuwakumbusha waamuzi watakaosimama katikati kuwa na mawasiliano na wenzake.
Maamuzi tata yanaweza kurudisha yale ya Yanga na Coastal Union, Yanga na Azam fc, Simba na Kagera Sugar.
Ili kutofikia huko, chondechonde waamuzi kuweni makini katika mechi za leo ili kutenda haki.
Kwa upande wa tatu wa mchezo kwamaana ya mashabiki nao lazima wawe wapesi kukubaliana na maamuzi.
Uamuzi ni taaluma ambayo mtu anakaa darasani kusomea sheria za mpira wa miguu.
Hapa mwamuzi anafundishwa namna ya kutafsiri sheria uwanjani. Kama mtu anasomea, basi anauelewa mkubwa wa sheria za mpira kuliko mtu yeyote Yule ambaye hajaenda darasani.
Kuna wakati mashabiki wanazomea waamuzi si kwasababu tu wamekosea sheria, bali kwasababu hawajui sheria fulani.
Ni ukweli uliowazi kabisa kuwa mashabiki wengi wamepitwa kushoto na baadhi ya sheria, hivyo hawana uwezo wa kutafsiri madhambi fulani uwanjani.
Wasomi wa sheria hizo wanapotafsiri, basi wanalipuka kwa kelele za kuzomea, bila kujiuliza je, wanazijua sheria hizo?.
Kikubwa kwa mashabiki leo hii ni kuwa na utulivu na uvumilivu wawapo uwanjani.
Wasiingie kwa mawazo ya lazima Yanga ishinde au Kagera Sugar, waende na akili ya kukubali matokeo kwasababu kila klabu ina haki ya kushinda.
Kagera kushinda wanaweza na Yanga wanaweza. Inapotokeoa timu moja inashindwa kutamba kwa mwenzake, basi wakubaliane na matokeo.
Mambo ya kufanya vurugu na kung`oa viti hayana nafasi kwasasa, lazima watu wawe waungwana.
Hakuna ulazima wa kufanya hayo, kila timu inaweza kupata matokeo.
Kukosea kwa waamuzi kupo na hata ulaya tunaona. Zipo njia za kufuata kama mnadhani timu yenu imeonewa katika mchezo na si kufanya fujo.