Mwandishi wa kitabu kinachoelezea namna watanzania na makampuni ya usambazaji ya hapa Tanzania yanavyoweza kushiriki, kuwezeshwa na kunufaika na sekta ya nishati ya gesi asilia hapa.Bi. Neema Lugangilra Apson akielezea maudhui ya Kitabu chake kwa wageni waalikwa (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa kitabu chake jana usiku jijini Dar es Salaam.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto) akiteta Jambo na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue jana wakati wa uzindizi wa kitabu cha “Local Content in Supplier Development” kilichoandikwa na Neema Lugangilra Apson.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto), Bi. Neema Lugangilra Apson (katikati) na Balozi wa Uingereza Dianna Melrose wakimsikiliza mgeni rasmi Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue (hayupo pichani) wakati wa uzinduzi huo jana usiku jijini Dar es salaam.
Mgeni Rasmi Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue akikata utepe kuashiria uzinduzi wa kitabu kinachoeleza namna watanzania na makampuni ya usambazaji yanavyoweza kushiriki, kuwezeshwa na kunufaika na sekta ya nishati ya gesi asilia hapa. Kulia ni mwandishi wa kitabu hicho Bi. Neema Lugangilra Apson.
Bi. Neema Lugangilra Apson akionesha kitabu chake kinachoitwa “Local Content in Supplier Development” kinachoelezea namna watanzania na makampuni ya usambazaji yanavyoweza kushiriki, kuwezeshwa na kunufaika na sekta ya nishati ya gesi asilia hapa.
Mgeni Rasmi Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue akipokea kitabu kinachoelezea namna watanzania wanavyoweza kushiriki na kunufaika na sekta ya nishati ya gesi asilia hapa nchini. Kulia ni mwandishi wa kitabu hicho Bi. Neema Lugangilra Apson.
Bi. Neema Lugangilra Apson akimkabidhi Binti yake Georgia Blessings Apson kitabu alichokiandika kinachoelezea namna watanzania na makampuni ya usambazaji yanavyoweza kushiriki, kuwezeshwa na kunufaika na sekta ya nishati ya gesi asilia hapa.
Msemaji wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Assah Mwambene (katikati) akifafanua jambo kwa Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue (kushoto) wakati wa uzinduzi wa kitabu cha Local Content in Supplier Development kilichoandikwa na Bi. Neema Lugangilra Apson jana Jijini Dar es Salaam, kulia ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa magazeti ya serikali (TSN) Gabriel Nderumaki.
Picha/Habari na Aron Msigwa na Eliphace Marwa – MAELEZO.
SERIKALI imewasisitiza wananchi hususan wafanyabiashara kote nchini kuwekeza katika utoaji wa huduma mbalimbali za kijamii katika maeneo yote yenye miradi ya gesi nchini.
Kauli hiyo imetolewa jana usiku jijini Dar es salaam na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue wakati wa hafla ya uzinduzi wa kitabu kilichoandikwa na mtanzania Bi. Neema Lugangira Apson chenye maudhui ya namna Kampuni za Kitanzania zilizojikita katika uwekezaji wa gesi zinavyoweza kushiriki ,kuendelezwa katika uwekezaji wa sekta ya gesi asilia nchini.
Akizungumza katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, balozi, makampuni yaliyowekeza katika sekta ya gesi na wadau mbalimbali Balozi Sefue amesema sekta ya gesi ni moja eneo lililo na fursa nyingi za uwekezaji kwa watanzania.
Amesema ni wakati wa wananchi kuziona fursa hizo na kuwekeza katika maeneo yote yanayohitaji uwekezaji wa huduma mbalimbali hususan za usambazaji na uuzaji wa vyakula, ujenzi wa nyumba za kulala wageni, uuzaji wa bidhaa muhimu, uuzaji wa bidhaa na vifaa vya gesi pamoja na vitu vingine vinavyohitajika katika maeneo ya miradi.
Ameeleza kuwa serikali imejipanga vizuri katika kuhakikisha kuwa sekta ya gesi inasimamiwa na kuendelezwa vizuri kisera na kufafanua kuwa tayari hatua mbalimbali zimekwisha chukuliwa kuhakikisha kuwa sekta ya gesi inakuwa na manufaa kwa wananchi na ustawi wa taifa.
“Katika hili serikali tumejipanga vizuri kwa kuhakikisha sekta hii inaleta manufaa kwa taifa, tumejifunza kupitia uzoefu mkubwa walioupata wenzetu hasa nchi kubwa zilizopiga hatua katika sekta ya gesi” Amesisitiza Balozi Sefue.
Balozi Sefue amewataka wafanyabiashara na wasambazaji wa ndani walioingia kwenye sekta ya nishati ya gesi na mafuta kufanya kazi zao kwa weledi mkubwa na kuzingatia ubora na viwango vinavyokubalika ndani na nje ya nchi na kuwasisitiza kuendelea kujifunza zaidi na kutafuta masoko ya bidhaa wanazozalisha ili kujenga uchumi imara.
Amesema serikali inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wanaowekeza katika sekta ya gesi na utafutaji wa mafuta nchini na kutoa wito kwa makampuni yanayojihusisha na sekta ya gesi kushirikiana na serikali katika mpango wa kuhakikisha shughuli wanazozifanya zinaboresha maisha ya watanzania.
Akizungumzia uzinduzi wa kitabu hicho Balozi Sefue amesema kuwa kitabu hicho kina mchango muhimu sana katika uendelezaji wa sekta ya gesi hapa nchini na kufafanua kuwa elimu iliyomo ndani ya kitabu hicho ni kwa manufaa ya watanzania wote.
Kwa upande wake mwandishi wa Kitabu hicho Bi. Neema Lugangira Apson akizungumza wakati wa uzinduzi wa kitabu chake amesema kuwa ameamua kuandika kitabu hicho kutokana na unyeti wa sekta ya Gesi asilia na umuhimu wa mchango wake kwa maendeleo ya taifa.
Amesema kitabu hicho kitachangia kuongeza uelewa wa masuala ya gesi kwa wananchi na makampuni ya kitanzania yanayowekeza katika sekta ya gesi kutokana changamoto iliyopo ya uelewa mdogo juu ya sekta hiyo jambo linalochangia ushiriki mdogo.
“Nimeandika kitabu hiki kutoa mchango wangu kuelezea namna kampuni za kitanzania zinavyoweza kushiriki kikamilifu na kuendelezwa ili zilete manufaa kwa watanzania, ugunduzi wa gesi umekuja wakati ambao watanzania tulio wengi hatujajiandaa vizuri na si kwamba hatuwezi katika hili jambo la msingi ni sisi wenyewe kuweka utashi na utayari wa kunufaika ” Amesisitiza.
Ametoa wito kwa makampuni ya ndani yanayojihusisha na sekta ya gesi kuungana uwekezaji yaweze kuwa na nguvu ya kushindana na makampuni kutoka nje ya nchi.
“Ni lazima tuhakikishe kuwa tunaimarisha makampuni yetu ya ndani ili tuweze kushindana na makampuni ya nje ikiwezekana mamlaka husika zitoe motisha kwa makampuni au wafanyakazi wanaofanya vizuri na wale wasiofanya vizuri waadhibiwe” Amesisitiza Bi. Neema.
Aidha amesema kitabu hicho kitapatikana bure ikiwa ni sehemu ya mchango wake kutoa maarifa kwa watanzania na wadau wote wa sekta ya gesi na kuongeza kuwa utaratibu wa kukichapisha kitabu hicho ambacho sasa kipo kwa lugha ya kiingereza unafanyika ili kiweze kupatikana kwa lugha ya Kiswahili.
Naye Balozi wa Uingereza nchini Tanzania ambaye ubalozi wake umehusika kutoa mchango wa ufanikishaji wa kitabu hicho Bi. Diane Melrose amemsifu mwandishi wa kitabu hicho na kueleza kuwa uzinduzi wa kitabu hicho ni fursa pekee ya wadau mbalimbali kujifunza mengi kuhusiana na sekta ya gesi nchini.
Amesema Tanzania na Uingereza zimekuwa na uhusiano wa karibu katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na kuongeza kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa wanufaa ya wananchi.
Katika hatua nyingine mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri wa Wachimba Madini Nchini (TPSF) Bw. Richard Kasesela akizungumza katika uzinduzi huo ameeleza kuwa kitabu hicho kitasaidia kuboresha sera zinazosimamia sekta hiyo hapa nchini.
Kuhusu sekta ya gesi nchini amesema kuwa wapo baadhi ya watu wamekuwa na mitazamo hasi juu kuhusu manufaa ya gesi kwa uchumi wa Tanzania ambao huilaumu serikali kwa kueleza kuwa gesi na mafuta havina mchango wowote kwa uchumi wa Tanzania jambo ambalo halina ukweli wowote kutokana na juhudi kubwa inayofanywa na serikali kuhakikisha sekta hiyo inawanufaisha watanzania.
Filed Under:
HABARI KITAIFA
on Friday, April 11, 2014