Dar es Salaam. Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia imesema ifikapo mwishoni mwa mwaka 2015 vijiji vyote nchini vitakuwa vimeunganishwa na huduma ya mawasiliano ya simu za mikononi.
Pia imesema mchakato wa kuzima mitambo ya analojia unaendelea kwa mikoa iliyosailia, Morogoro, Tabora, Singida, Musoma, Kigoma, Kahama, Iringa, Songea na Lindi.Hadi sasa mikoa ambayo haitumii tena analojia na imeanza kutumia mitambo ya dijitali ni Dar es Salaam, Mwanza, Tanga, Mbeye, Arusha na Dodoma.
Hayo yalisemwa juzi na Waziri wa wizara hiyo, Profesa Makame Mbarawa wakati akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia uliokuwa ukijadili mambo mbalimbali yaliyojitokeza katika kipindi cha mwaka 2013/14.
Profesa Mbarawa alisema tangu mwaka 2005 hadi sasa, watumiaji wa huduma za mawasiliano wameongezeka kutoka laini za simu za mkononi milioni 2.9 milioni hadi milioni 27.5 Desemba mwaka jana.
“Tunajitahidi kuhakikisha ifikapo mwishoni mwa mwakani, huduma za mawasiliano ziwe zimefika vijijini ili kurahisisha maendeleo ya jamii na kuwavutia wawekezaji wengi kuwekeza maeneo hayo,” alisema Profesa MbarawaKuhusu uzimaji wa mitambo, Profesa Mbarawa alisema licha ya changamoto mbalimbali zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa awamu ya kwanza, mafanikio makubwa yameonekana.
