WAZIRI wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangala amelipongeza Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa kuviunganisha vyombo vya habari anuai nchini Tanzania kupitia tasnia ya michezo.
Dk. Mukangala ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam katika hotuba yake iliyosomwa na Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia kwa niaba ya waziri, alipokuwa akifunga rasmi Mashindani ya 11 ya NSSF yanayoshirikisha vyombo vya habari anuai katika mchezo wa mpira wa miguu na mpira wa pete kwa wasichana.
Dk. Mukangala alisema kwamba mashindano hayo yamekuwa yakivikutanisha vyombo anuai vya habari kutoka Tanzania Bara na Visiwani hivyo kujenga uhusiano mzuri kwa washiriki kupitia michezo, huku yakiimarisha uhusiano kati ya vyombo hivyo na shirika la NSSF ambalo hudhamini mashindano hayo kila mwaka kwa muda wa miaka 11 mfululizo hivi sasa.
"Hakuna ubishi kwamba miaka 11 sio michache kwa kuendesha mashindano kama haya, lakini kwa sababu uongozi wa NSSF unaheshimu na kukubali nafasi ya vyombo vya habari katika kuelimisha jamii ni wazi kwamba mtaendelea kutenga bajeti ya mashindano haya kila mwaka, " alisema Dk. Mukangala.
Aidha aliwapongeza washindi wa mwaka huu kwa jitihada na nidhamu ya mchezo waliozionesha hadi kufanikiwa kutwaa ushindi, hivyo kuwataka wanahabari wote kuendelea kuyatumia mashindano hayo kwa kujenga mahusiano mazuri na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii.
Mwaka huu timu ya Kampuni ya Bussnes Times Limited (BTL) imefanikiwa kutwaa kombe la mpira wa miguu na kuzawadiwa fedha shilingi milioni nne na nusu baada ya kuishindilia Changamoto mabao matatu kwa mtungi, nafasi ya pili ilichukuliwa na timu ya Changamoto na kujinyakulia kikombe pamoja na kitita cha shilingi milioni tatu na nusu.
Mshindi wa tatu mpira wa miguu imeibuka timu ya wenyeji wa mashindano hayo NSSF baada ya kuifunga timu ya Mwananchi, hata hivyo NSSF walichukua kikombe na kusamehe kitita chao cha shilingi milioni 2 kilichokabidhiwa mshindi wa nne, yaani Timu ya Mwananchi.
Neema ya mashindano hayo mwaka huu iliiangukia kampuni ya BTL ambapo kwa upande wa mpira wa Pete pia timu ya wasichana ya kampuni hiyo ilifanikiwa kutwaa ubingwa na kukabidhiwa kombe na fedha shilingi milioni 4, nafasi ya mshindi wa pili imechukuliwa na timu ya Habari kutoka Zanzibar na kujinyakulia kiasi cha shilingi milioni tatu na nusu.
Washindi wa tatu mpira wa pete imeibuka timu ya NSSF ambao walitwaa kombe bila fedha ambazo zilichukuliwa na mshindi wa nne (Mwananchi). Kikombe cha nidhamu kimenyakuliwa na timu ya Tumaini wamiliki wa Redio na TV Tumaini pamoja na gazeti la Tumaini Letu.
Jumla ya timu 20 za mpira wa miguu na 18 za mpira wa pete zimeshiriki mashindano hayo kwa mwaka huu idadi ambayo inazidi kuongezeka kila mwaka tangu kuanza kwa mashindano hayo.
Hafla ya kufunga mashindano hayo iliyofanyika katika viwanja vya Sigara (TCC) jijini Dar es Salaam pia ilihudhuriwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya NSSF, Abubakar Rajabu, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Dk.
Ramadhani Dau viongozi waandamizi wa shirika la NSSF pamoja na wageni mbalimbali waalikwa. Nahodha wa timu ya mpira wa pete ya Business Times Limited akikabidhiwa kikombe mara baada ya timu hiyo kuibuka mabingwa.
Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia (mwenye traksuti nyeusi) akikabidhi kikombe kwa nahodha wa timu ya mpira wa miguu ya Business Times Limited baada ya timu hiyo kuibuka mabingwa wa mpira wa miguu. Wengine ni viongozi wajuu wa NSSF wakishuhudia.