Kamanda wa polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz amewatahadharisha wazazi wenye watoto wadogo kuwaelimisha wafanyakazi wa ndani kutowakabidhi watoto wao kwa watu wasiowafahamu.
Tahadhari hiyo imekuja baada ya watu watatu wakiwa na pikipiki mbili, kufanya jaribio la kumteka mtoto wa mwandishi wa gazeti hili mkoa Kilimanjaro, Rehema Matowo katika tukio la jana saa 7:00 mchana.Watu hao walifika nyumbani kwa mwandishi huyo saa 7:00 mchana na kumweleza mfanyakazi wa ndani kuwa wametumwa na baba mzazi wa mtoto huyo ili wamchukue kutoka Soweto na kumpelekea katikati ya mji.
“Aliwauliza mbona baba wala mama hajapiga simu? Watu hao wakasisitiza wametumwa kumchukua mtoto huyo tena wakimtaja kwa jina mtoto huyo na jina la baba,” alisema Rehema.
Mtoto huyo ana umri wa miaka miwili na miezi minane.Hata hivyo mfanyakazi huyo aliwatilia shaka watu hao na kurudi ndani kisha kufunga geti la nyumba hiyo lakini watu hao waligonga geti hilo mara kadhaa wakisisitiza kupewa mtoto.
Wakati watu hao wakiendelea kugonga geti hilo, mfanyakazi huyo alimpigia simu mwandishi huyo na kumweleza, ambapo alimtahadharisha kutofungua geti hilo kwa vile ni jambo la ajabu.
“Tumeondoka na mume wangu asubuhi kwenda ofisini na kila mmoja anafanya kazi ofisi tofauti. Isingewezekana kumhitaji mtoto bila kunijulisha mimi na nilipomweleza naye alishtuka sana,” alisema.
Kutokana na tukio hilo, Kamanda Boaz aliwatahadharisha wazazi kuwa makini, ikiwamo kuwapa elimu wafanyakazi wao ili kuchukua tahadhari wakati wanapokutana na matukio yasiyo ya kawaida.