Baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu Bara huku Mbeya City ikionyesha ushindani wa hali ya juu kwa timu kongwe kwenye ligi hiyo, wamiliki wa timu hiyo ambao ni Halmashauri ya Jiji la Mbeya wamewatangazia donge nono la mshahara kwa wachezaji na benchi la ufundi katika msimu ujao wa ligi hiyo.
Meya wa Jiji la Mbeya, Athas Kapunga alisema kauli hiyo kwenye hafla fupi ya kuvunja rasmi kambi ya timu hiyo iliyofanyika jijini Mbeya usiku wa Jumamosi iliyopita katika Ukumbi wa Hoteli ya Mount Living Stone.
Kapunga alisema kuwa baada ya kumazilika kwa Ligi Kuu huku City ikipata mafanikio makubwa na vijana wao kuonyesha umahiri ni wazi kuwa kuna timu zimepanga kuivuruga timu kwa kuwachukua wachezaji hao kwa kigezo cha kuwalipa vizuri, hivyo na wao wanajipanga na kuangalia namna watakavyowalipa vizuri zaidi kwenye msimu ujao.
“Bodi ya michezo itakaa na uongozi wa Halmashauri ya Jiji na kuangalia namna ya kuwalipa mshahara vizuri zaidi vijana wetu na hili linawezekana tena zoezi hili linaanza kutekelezwa msimu ujao wa ligi na nina hakika hakuna mchezaji atakayedanganyika kwenda timu nyingine kwa kisingizio cha mshahara,
” alisema Meya Kapunga.Awali, akizungumza machache, mgeni rasmi katika hafla hiyo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya, Mariamu Mtunguja, alimtaka kocha Juma Mwambusi kutanguliza zaidi uzalendo ili asije akaikacha timu hiyo na kwenda timu nyingine baada ya kuonesha mafanikio makubwa kwa Mbeya City.