Moto Uliozuka Hospitalini wauwa watu 21 Nchini Korea Kusini. Wagonjwa wapatao 20 pamoja muuguzi wameuawawa baada ya moto mkubwa kuwaka hospitalini katika jimbo la Janseong nchini Korea Kusini, huku wengine 6 wakiwa hali mahututi baada ya moto huo katika hospitali ya Hyosarang iliyoko kilomita 300 kusini mwa Seoul.
Wengi wa walioaga dunia wanafikiriwa kuwa wazee wenye umri wa kati ya miaka 70 na 80 na wasioweza kutembea. Maafisa walisema kuwa wengi waliokufa walikosa hewa kutokana na gesi zenye sumu. Moto huo ulizimwa kwa takribani nusu saa. Moto huo ulianza muda mfupi tu baada ya saa sita usiku katika hilo jumba lenye orofa tatu.
Vyombo vya habari vinaarifu kuwa wengi wa wagonjwa waliokuwa katika orofa ya juu ya jumba hilo walishindwa kujiokoa kwa sababu vyuba vyao vilikuwa vimejaa moshi uliotokana na moto huo. Muuguzi huyo aliyekufa alikuwa akijaribu kuzima moto kwa kutumia kizima moto kulingana na shirika la Agence-France Presse.
Ripoti ya shirika la Yonhap ilisema kuwa polisi walisema kuwa jumba hilo lilikuwa limefanyiwa uchunguzi wa kiusalama majuzi. Mkurugenzi wa hospitali hiyo Lee Hyung Seok aliomba msamaha na kuwaambia wanahabari kuwa alikuwa ametenda dhambi kubwa, na kuwa hangetoa visababu wakati watu wameaga dunia.
Tukio hili limekuja wakati wananchi wa Korea kusini wakiendelea kuomboleza vifo vya zaidi ya watu 300 waliofariki katika ajali ya feri iliyotokea mwezi uliopita. Rais wa taifa hilo Park Geung-Hye ameliomba taifa radhi kirasmi kwa ajali hiyo ya feri, huku akiahidi kuimarisha viwango vya usalama.
Waziri mkuu Chung Hong-won wakati huo alijiuzulu kwa madai ya jinsi serikali ilivyokuwa ikikabiliana na majanga. Ajali hiyo ya hospitali pia imetokea siku moja tu baada ya watu 7 kuuwawa na wengine 20 kujeruhiwa katika mkasa wa moto uliozuka katika kituo cha mabasi jijini Goyang.