Rais Jakaya Kikwete ameahidi kuendelea kuimarisha huduma za afya hasa ya mama na mtoto ili kupunguza vifo hapa nchini.
Kikwete ametoa ahadi hiyo nchini Canada wakati wa mkutano kuhusu afya ya mama na mtoto na kupokea msaada wa Dola za Marekani 3.5 bilioni ambazo ni zaidi ya Sh5.6 trilioni kutoka kwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Stephen Harper kwa lengo la kuimarisha lishe na kupunguza magonjwa.
Akipokea msaada huo jijini Toronto, Rais Kikwete alisema kuwa, kwa kushirikiana na jumuiya na makampuni ya kimataifa, washirika wa maendeleo na sekta binafsi Tanzania imefanikiwa kupunguza vifo vya watoto kama ilivyoainishwa na Umoja wa Mataifa katika malengo ya milenia.
“Katika kufikia malengo, Tanzania imefanikiwa kupunguza vifo vya watoto wachanga toka 191 mpaka 21 kati ya 1,000 huku vile vya watoto chini ya miaka mitano vikipungua kutoka 115 mpaka 54 kati ya 1,000,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:
kuwa serikali imekuwa ikichukua hatua za makusudi kuhakikisha kuwa huduma za afya zinaboreshwa kote nchini.
Katika mkutano huo uliohudhuriwa pia na Malkia Rania wa Jordan na Melinda Gates, Rais alisisitiza kuwa serikali itaendelea kuongeza bajeti na kuomba ushirikiano wa wadau mbalimbali, wa ndani na nje, ili kufikia malengo hayo.
“Serikali imefanikiwa kuongeza bajeti ya afya kutoka Sh271 bilioni mwaka 2007 mpaka Sh1.4 trilioni mwaka 2013 sambamba na kujenga zahanati 1,640, vituo vya afya 122 na hospitali mpya 19 ikiwa ni pamoja na kuboresha na kupandisha hadhi za hospitali za wilaya na mikoa,” aliongeza Rais.
Rais pia aliueleza mkutano huo kuwa serikali yake imepandisha hadhi za zahanati na vituo vya afya, ili viweze kutoa huduma ya ukunga na kutoa mafunzo kwa watumishi, huku pia ikiboresha upatikanaji wa dawa na vifaa.