Serikali ya Uturuki inatarajia kujenga Kituo Maalumu kwa ajili watoto zaidi ya 400 wenye ulemavu wa ngozi nchini (Albino) kinachotarajiwa kuwaweka katika mazingira salama kutokana na kukabiliwa na vitisho vya mauaji yanayohusishwa na imani za kishirikina huku wengine wakipoteza maisha bila hatia.
Hatua hiyo imekuja ikiwa imepita wiki moja tangu mabalozi 12 wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini walipomtumia Waziri Mkuu, Mizengo Pinda barua ya wazi wakimtaka kuchukua hatua stahiki kwa watu waliofanya mauaji ya albino wilayani Bariadi, mkoani Simiyu.
Akizungumza jana kwenye mkutano na waandishi pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Ahmet Davutoglu, Waziri wa Mambo ya Nje wa nchini, Benard Membe alisema kituo hicho ujenzi wake unatarajiwa kuanza rasmi hivi karibuni.
Waziri huyo alifafanua kuwa kituo hicho kimeshatengewa kiwanja chenye ukubwa wa hekari 39 maeneo ya Barabara ya Bagamoyo.
Kituo hicho kitajengwa shule, hospitali kwa ajili ya huduma za afya na hosteli ya watoto hao. Kituo hicho kinaweza kuleta afuheni kwa walemavu ambao wamekuwa akiishi kwa hofu ya kuuwawa.
Katika tukio la Mei 12 mwaka huu ambalo lilipelekea mabalozi hao kuandika barua kwa waziri mkuu ni lile la albino mmoja aliyetajwa kwa jina la Munghu Lugata mkazi wa Bariadi mkoani Simiyu kuuawa kikatili na watu wasiojulikana.
Mauaji hayo yaliongeza idadi ya maalbino waliouwa kikatili nchini kufikia 73 tangu mwaka 2000 huku wengine wakikatwa baadhi ya viungo vyao vya mwili na kutishiwa maisha.
Jambo hilo limekemewa vikali na Waziri Davutoglu aliyesema ulemavu wa ngozi unaweza kumpata mtu yeyote hivyo jamii inapasaswa kuwapenda na kuwajali watoto hao. “Jamani inatakiwa kuelewa hakuna tofauti kati ya albino na mtoto wa kawaida na tukumbuke kuwa binadamu wote ni sawa”.