Serikali imekamilisha kanuni za tozo zitakazowabana waajiri wote wa sekta binafsi nchini kuchangia uendeshaji wa mfuko wa fidia kwa wafanyakazi.
Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka alisema hayo bungeni jana wakati akiwasilisha Bajeti ya Wizara yake kwa Mwaka wa Fedha wa 2014/2015.
Kabaka alisema suala hilo ni takwa la kisheria chini ya kifungu 74(10 cha Sheria ya Mfuko wa Fidia ya Wafanyakazi ya mwaka 2008).
Mfuko huo utaendeshwa kwa kutumia mfumo wa bima na pensheni kwa kutoa mafao kwa watumishi watakaoumia, kupatwa na magonjwa yanayosababishwa na mazingira ya kazi au kufariki sehemu ya kazi.
Katika mwaka wa fedha wa 2014/2015, wizara itaendelea kuratibu juhudi za Serikali za kukuza ajira nchi, ambapo katika kipindi hicho ajira 700,000 zitazalishwa.
Waziri Kabaka alisema ajira hizo mpya zitategemea kuzalishwa kutokana na utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na taasisi za umma.
Miradi hiyo pia inatekelezwa na Programu ya kukuza ajira kwa vijana pamoja na hatua mbalimbali za uwekezaji kupitia Kituo cha Uwekezaji (TIC), Mamlaka ya Maeneo Huru ya Biashara (EPZA) na sekta binafsi.
Waziri Kabaka alisema katika mwaka wa Fedha 2013/2014, ajira 630,616 zilizalishwa hadi kufikia Aprili mwaka huu.Sekta zilizotoa ajira hizo na kiwango cha ajira kikiwa kwenye mabano; Kilimo(130,974), Elimu (36,073), Ujenzi wa Miundombinu(32,132), Afya (11,221).
Kwa mujibu wa Kabaka, sekta nyingine ni Nishati na Madini (453), Tasaf (86,860), sekta nyingine Serikalini(2,321), sekta binafsi (211,970) na mawasiliano (13,619).
Viwanda vidogo na vya kati (SME) 7,192, EPZ 26,381 na miradi kupitia kituo cha Uwekezaji (TIC) 149,594.