Kigoma. Wananchi mkoani hapa wametakiwa kufanya usafi wa mazingira ndani na nje ya kaya zao, ili kuepuka ugonjwa wa dengue kubainika kuwa na mgonjwa mmoja.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Dk Leonard Subi alisema hivi sasa kuna mgonjwa mmoja wa dengue kutoka Wilaya ya Buhigwe.
Alisema mgonjwa huyo anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Misheni ya Heru, baada ya kuambukizwa kirusi cha mmbu aina ya Adesy ambaye ameambukizwa ugonjwa huo.
“Mgonjwa huyu alitoka Dar es Salaam, alikuja Kigoma kwa lengo la kusalimia ndugu na jamaa.
Wakati huohuo akapatwa na homa ya ghafla na baada ya kuchukuliwa vipimo akagundulika ana ugonjwa wa dengue,” alisema Dk Subi.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Kanali mstaafu Issa Machibya aliwaonya wananchi kuepuka kupokea taarifa zisizo na utafiti wa uhakika kutoka wizara husika kuhusu tiba zinazotolewa katika mitandao ya jamii, kwa kubainisha tiba bandia ya ugonjwa huo.
Machibya aliwataka watu wanapoona dalili kama vile kutoka damu sehemu za wazi, kuchoka kwa viungo vya mwili na homa kali waende haraka kwenye vituo vya afya kwa uchunguzi.