Tarime. Katika Kijiji cha Gomsala, Tarime mkoani Mara yupo
Matuma Marwa (22), ambaye hakuwahi kufikiria kwamba siku moja atakuwa
mlemavu pamoja na kuwa kila binadamu aliye hai ni mlemavu mtarajiwa.
Marwa alipatwa na ulemavu wa mguu Oktoba 9, mwaka jana, baada ya kupigwa risasi na polisi kwenye paja.
“Tulikuwa tunaelekea shambani, tukasikia milio ya
risasi ikielekezwa tuliko sisi, risasi moja ilinipata kwenye paja na
tangu wakati ule hadi sasa mguu wangu hauko sawa,” alisema Marwa na
kuongeza:
“Kazi yangu ni mkulima, ila kwa sasa nashindwa kulima kwa kuwa mguu bado unauma.”
Marwa ni miongoni mwa watu waliopatwa na madhila yatokanayo na vita ya rasilimali baina ya wananchi na wawekezaji.
Marwa anaishi katika kijiji kilicho kandokando ya mgodi wa dhahabu wa North Mara.
Mgodi wa North Mara unamilikiwa na Kampuni ya
African Barrick Gold tangu 2006 ilipoununua kutoka kwa Kampuni ya Placer
Dome Tanzania, iliyokuwa ikimilikiwa na Afrika Mashariki Gold Mines.
Taarifa rasmi kutoka katika vijiji vinavyozunguka
mgodi huo, zinaonyesha kuwa, mbali na waliojeruhiwa na kupata ulemavu wa
kudumu, pia wapo waliopoteza maisha kutokana na kupigwa risasi na
polisi wanaolinda usalama katika migodi hiyo.
Matukio hayo na mengine ya unyanyasaji,
yanawafanya wakazi wa maeneo haya kuchukulia uwepo wa madini ya dhahabu
kama kero kwao na siyo neema au baraka kama ilivyotarajiwa.
Watu 24 wanadaiwa kwamba wamekwisha uawa kwa
kupigwa risasi katika matukio, akiwamo mkazi wa Kijiji cha Nyangoto,
Ryoba Maseke ambaye alipigwa risasi Julai 12, 2012.
Shangazi wa Maseke, Suzana Mwita anasema, marehemu
alikuwa mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya sekondari ya
Mugumu, Serengeti na alifika kijijini kusalimia ndugu zake na hapo ndipo
mauti yalipomkuta.