Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam imewaruhusu kwenda kutibiwa nje ya nchi Mawaziri Waandamizi wa zamani ambao ni Basil Mramba na Daniel Yona wanaokabiliwa na tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka.
Matumizi hayo mabaya ya madaraka yanadaiwa kuisababishia Serikali hasara ya Sh. bilioni 11.7 kwa kutoa msamaha wa kodi.
Uamuzi huo umetolewa leo mahakamani hapo na Jaji John Utamwa baada ya washtakiwa hao kuwasilisha maombi ya kwenda kutibiwa nje ya nchi ambapo Upande wa Jamhuri ulidai kuwa hauna pingamizi na maombi hayo.Baada ya kusikiliza ombi hilo Jaji Utamwa alisema mahakama inawaruhusu washtakiwa kusafiri kwenda nje ya nchi kutibiwa na kwamba pamoja na ruhusa hiyo amewataka Mramba na Yona kuwepo mahakamani siku ya kusikiliza kesi hiyo Aprili 22 mwaka huu.
Katika kesi hiyo inayowakabili Mramba na Yona piamshtakiwa mwingine ni Katibu Mkuu wa zamani wa Wizara ya Fedha Gray Mgonja,Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa Aprili 22 hadi 25, mwaka huu.
Katika kesi ya msingi washtakiwa wanadaiwa kuwa kati ya Agosti mwaka 2002 na Juni 14 mwaka 2004 jijini Dar es Salaam wakiwa watumishi wa umma kama mawaziri na katibu mkuu walitumia vibaya madaraka.
Ilidaiwa kuwa kwa kupitia kampuni ya Alex Stewart (ASSAYERS) ya Uingereza iliyoingia mkataba wa ukaguzi wa madini ambapo kwa kupitia kampuni tanzu ya Alex Stewart ( ASSAYERS) Government Business Corporation waliingia mkataba kukagua kiwango cha uzalishaji wa madini ya dhahabu kinyume cha Sheria ya Manunuzi ya Umma.