Dar es Salaam. Chuo cha Bandari Dar es Salaam kimeshauriwa kufanya juhudi ili kije kuwa chuo kikuu kwa lengo la kuongeza ufanisi kwenye soko la ajira, hususan katika fani ya usimamizi, upakiaji na usafirishaji mizigo bandarini.
Ushauri huo ulitolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi Bandari Tanzania, Johnson Noni wakati wa maadhimisho ya maafali ya 14 yaliyofanyika mwishoni mwa wiki chuoni hapo.
Noni alisema kuwa, wakati umefika kwa chuo hicho kupanua wigo wa kitaaluma kwa kuongeza ngazi ya shahada kwa kozi wanazotoa ili kuinua viwango vya wahitimu na utendaji kazi.
“Bandari ndiyo chuo pekee nchini kinachotoa stashahada katika fani za bandari. Hivyo, sioni kwa nini kisikuze stashahada hizi na kuzifanya ziwe shahada. Hii ni changamoto nawaachieni,” alisema Noni.
Kadhalika, Noni alitia mkazo wa kuzingatia viwango vya elimu vinavyotolewa chuoni hapo katika kozi za uhandisi, usafirishaji, upakiaji na upakuaji wa mizigo bandarini ili kupata wahitimu bora.
“Viwango vya utoaji elimu na mafunzo vidumishwe, hakikisheni chuo kinasajili wanafunzi wenye sifa zinazotakiwa. Fanyeni uhakiki wa vyeti kwa wanafunzi,” alisema Noni.
“Kama mmeweza kufanya mambo makubwa kiasi hiki, sioni kama mtashindwa kufikia malengo ya kutoa shahada ili kuwavutia watu wengi kujiunga na chuo, jambo ambalo litaleta tija kwa taifa,” alisema.
Alishauri pia chuo kuajiri walimu wenye sifa na uwezo wa kufundisha, kwani kwa kufanya hivyo kutasaidia kuzalisha wanafunzi bora katika fani ya mambo ya bandari.
Kaimu mkuu wa chuo hicho, Anthony Mateza alisema licha ya changamoto za upungufu wa majengo na walimu, chuo kimeweza kufungua matawi matatu yanayotoa mafunzo ya bandari katika Mikoa ya Mtwara, Tanga na Dar es Salaam.
“Tunaendelea kuongeza idadi ya matawi kutegemeana na mahitaji na sasa tuko kwenye mchakato wa kufungua tawi lingine la chuo Mkoa wa Mwanza,” alisema.
Alisema dhamira ya chuo ni kujipanua kadri kitakavyoweza kupata nafasi na hiyo itatokana na kuwepo na uongezeko la wanafunzi wanaotaka kujiunga.