Hivi karibuni Mjumbe wa Tume ya Marekebisho ya Katiba (jina limehifadhiwa) aliwahi kuhojiwa na mwandishi wa makala haya kuhusu matarajio ya Watanzania kuhusu Katiba Mpya na matumizi ya Kiswahili.
Naye alisema: “Nawataka wajumbe wa Bunge la Katiba watakaokwenda Dodoma kutumia lugha sahihi inayoeleweka kwa wananchi, badala ya kuchanganya lugha. Wajumbe wasichanganye lugha ‘Kiswanglish’ kama ilivyotokea katika mikutano mingine ya kitaifa hata bungeni.
Hali hii inajitokeza sana siku hizi katika vikao mbalimbali vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kiswahili ndiyo lugha rasmi ya Bunge hilo lijalo na tungependa wabunge wazingatie hilo, maana tunaona baadhi ya mawaziri na wajumbe wengine wakichanganya lugha.”
Kauli aliyoitoa mjumbe huyu ni ya kupigiwa mfano kwani ametoa ya rohoni. Ni mzalendo kwelikweli, kwani ameweka mbele masilahi ya Watanzania wote. Hawa wajumbe wanawawakilisha Watanzania 45 milioni, ambao wana haki ya kujua hatima ya nchi yao kwani yatakayoamriwa katika Bunge hilo la Katiba yatamgusa kila mwananchi.
Katiba hii ni ya kihistoria tofauti na zile zilizotangulia ambazo zimekuwa zikifanyiwa marekebisho bungeni bila wananchi kujua kinachoendelea kwani hawakushirikishwa kuzitunga.
Matumizi ya lugha fasaha na sanifu ya Kiswahili wakati wa mijadala ya Bunge la Katiba ni jukunu la kila mjumbe. Kwa wale wenye matatizo kidogo kwa maana ya wasomi walioathiriwa na lugha za kigeni wajitahidi kujiandaa zaidi kabla ya kuzungumza. Wajitayarishe kwa kutumia kumbukumbu za kuwaelekeza ni nini cha kuzungumza, wakitumia mwongozo uliowekwa. Wenzetu wasomi wanatumia maneno ‘talking notes’ kama kiongozi cha mazungumzo.
Maandalizi ya aina hii yatawawezesha wajumbe kutumia lugha ya Kiswahili bila hofu, akiamini kuwa wasikilizaji watafaidika na hoja zake.
Mjumbe huyu wa Bunge Maalumu la Katiba ametoa rai ya kuachana na tabia ya kuchanganya lugha katika mazungumzo ambayo imeshamiri kwa Watanzania, wasomi walio wengi.
Hili ni suala lililoguswa na wengi kwamba wabunge wakiwamo mawaziri huchanganya maneno na hata vifungu vya maneno ya kigeni wanapochangia hoja bungeni. Inawezekana wanafanya hivyo kwa kukosa maneno ya Kiswahili yanayofaa, lakini wanakera zaidi wanapozungumza. Kwa mfano anaweza kusema;
“Wananchi wa jimbo langu hawana ‘idea’ ya mradi huu wa umwagiliaji ambao ‘donors’ wametoa zaidi nusu ya fedha zote.”
Wako baadhi ya wasikilizaji wataelewa kilichotamkwa bungeni, lakini kwa jumla ni makosa kutumia maneno kama ‘idea’ na ‘donors’.
Kwa utafiti wangu mdogo nimegundua kuwa hatakuwapo Mjumbe wa Bunge la Katiba mwenye elimu chini ya kidato cha nne.
