Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 Kama ilivyorekebishwa.Katiba inazungumzia Haki na Wajibu Muhimu.Inampa kila raia wa Tanzania haki za msingi zifuatazo kama zilivyoainishwa katika Ibara ya 12 mpaka ibara ya 29.HAKI HIZI NIPAMOJA NA:
1- Haki ya Usawa, ambayo inajuamuisha haki ya usawa wa binadamu( Ibara ya 12) na usawa mbele ya sheria( Ibara 13)Haki hii inapunguzwa makali yake kwa kuwa na kinga mbali mbali ambazo zipo kisheria mfano kinga za wabungewakiwa katika mijadala bungeni makosa wanayoyafanya katika mijadala hiyo hawawezi kushitakiwa.
2- Haki ya kuishi , hii inajumuisha haki ya kuwa hai( Ibara ya 14) na haki ya uhuru wa mtu binafsi ( Ibara ya 15)Haki ya kuwa hai ilipata kutafsiriwa kwenye kesi ya R v. Mbushuu Dominic Mnyaroge ( Reported case)Hata hivyo ni maoni ya Mwandishi kuwa Ibara hii ya katiba ina mapungufu hasa tukizingatia kifungu cha 196 cha sheria ya Makosa ya jinai amabacho kinatoa adhabu ya kifo kwa mtu aliyepatikana na hatia ya kuua kwa kukusudia.Na kwa mantiki hiyo basi ni wazi kifungu hicho hapo cha sheria ya makosa ya jinai kinaweza kuonekana kuwa kinakinzana na Ibara hiyo ya Katiba.
Ni wazi kuwa katiba ilipaswa katika Ibara hii iweke wazi kuwa haki ya kuishi inaweza kuondolewa pale mtu atakapopatikana na hatia ya kuua kwa kukusudia. Soma pia Ibara ya 31(3), hii inazungumzia uwezekano wa mtu kutolewa haki yake ya kuishi, Ibara ndogo hii inasema wakati wa vita ikiwa na maana kwamba kifo wakati wa vita na tunaweza kuweka msisitizo kuwa na wala si kunyongwa kwa kosa la kuua kwa kukusudia katika mazingira mengine yale.
Haki ya Uhuru wa mtu binafsi ilijadiliwa katika shauri ( kesi ya) la Daudi Pete v. D.P.P ( Reported ) kesi hii ilihusu haki ya dhamana. Kwa mantiki hiyi ibara hii inahusu haki ya dhamana ambayo imewekwa wazi na Sheria za Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya Mwaka 1985.
Haki hii ya uhuru wa mtu binafsi inaweza kuondolewa katika utaritibu wa kufuata sheria ( Ibara ya 15 (2)(a)) na katika kutekeleza hukumu, amri au adhabu iliyotolewa na mahakama kutokana na shauriau na mtu kutiwa hatiani kwa kosa la jinai ( Ibara ya 15 (2) (b)).Haki ya kuishi pia inajumuisha haki ya faragha na ya usalama wa mtu ( Ibara ya 16), pamoja na uhuru wa mtu kwenda atakako katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ( Ibara ya 17)Ibara hii inaweza kudhaniwa au kuonekana kana kwamba inakinzana na sheria zingine mfano haki ya kupata habari na Sheria ya uhuru wa vyombo vya habari. Hata hivyo mjadala huo utajadiliwa kwa kina siku nyingine.
3- Haki ya Uhuru wa Mawazo.Haki hii inajumuisha uhuru wa kutoa maoni ( Ibara ya 18). Walio wengi watakumbuka mijadala iliyokuwepo miaka ya hivi karibuni kuhusu NGO moja kwa jina la Haki Elimu na kiujumla wake mjadala huo ulikuwa ukihusisha tafsiri ya ibara hii. Haki ya uhuru wa mawazo pia inajumuisha uhuru wa mtu kuamini dini atakayo ( Ibara ya 19), uhuru wa mtu kushirikiana na wengine ( Ibara ya 20) na uhuru wa kushiriki shughuli za umma ( Ibara 21) Hata hivyo haki hizi hazitafsiriwi kama ni mwanya wa watu kukashifiana au kudharauliana.
4- Haki ya kufanya kaziHii inajumuisha, haki ya kufanya kazi ( Ibara ya 22), haki ya kumiliki mali ( Ibara ya 23),hata hivyo Ibara hii haizuii sheria zingine kufanya kazi maana inatoa mwanya kwa sheria zingine pia kutumika. Haki ya kufanya kazi pia inajumuisha pia haki ya kupata ujira wa haki(Ibara ya 24). Haki hii ilijadiliwa katika shauri la Lohay Akonaay v. A.G ( Reported).Hizi ndizo haki za raia katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hata hivyo kuna wajibu wa JamiiI- Wajibu wa kushiriki kazini ( Ibara 25)II- Wajibu wa kutii sheria za nchi ( Ibara ya 26). Na ikumbukwe kuwa sheria inachukulia ya kuwa kila raia au mtu yeyote aliye ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anajua sheria za Tanzania.
5- Wajibu wa kulinda mali ya umma hili ni jukumu la kila raia katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ( Ibara ya 29)
6- Ulinzi wa Taifa ni jukumu la kila raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ( Ibara ya 28)Hata hivyo haki hizi zilizoanishwa katika ibara ya 12-28 ya Katiba zina masharti yake ya Jumla kama yalivyo ainishwa katika Ibara ya 29,ambayo inaweka wazi kuwa kila raia ana haki ya kufaidi haki hizo za msingi za binadamu, bila kujali dini, rangi,itikadi wala kabila, na pia ni budi kwa kila raia akazingatia ya kuwa haki na uhuru kama ilivyoainishwa kwenye ibara za 12-28 zinatumiwa bila kuathiri au kuingilia haki au uhuru au maslahi ya watu wengine.
Na kama hiyo haitoshi Ibara ya 30(2) inaeleza kinagaubaga kuwa haki na uhuru kama ilivyoainishwa katika ibara ya 12 -28 zitatumika kwa kuzingatia sheria zingine zilizotungwa, kwa mantiki hiyo basi sheria zingine haziharamishwi na hivyo basi zinaweza kupunguza au kuzuia haki hizi kwa njia moja au nyingine na hii yote ikiwa ni katika kuhakikisha kwamba haki na uhuru wa watu wengine au maslahi ya umma haviathiriwi na matumizi mabaya ya uhuru na haki za watu binafsi ( Ibara ya 30(2) (a).
Unaweza ukasoma Ibara yote ya 30 ufahamu zaidi na pia unaweza kusoma ibara ya 31 ambayo inazungumzia ni wakati gani haki hizi zinaweza kukiukwa, ibara inasema ni wakati wa hali ya hatari , n.k.
