Watu wanaodaiwa kuwa majambazi wameiba magari mawili aina ya Land cruiser mali ya taasisi ya taifa ya utafiti wa magonjwa ya binadamu (NIMR) baada ya kuwalaghai askari waliokuwa lindo kisha kuwapa chakula kinachodaiwa kuwa kilikuwa na dawa za kulevya na kufanikiwa kuyachukua kiurahisi.
Mkuu wa kituo cha utafiti wa magonjwa ya binadamu wilayani Muheza Dr, William Kisinza amesema tukio hilo limetokea majira ya alfajiri baada ya majambazi hao kuwapa chakula na kinywaji kinachodaiwa kuwa na dawa za kulevya ndipo walipochukua funguo ya geti na kufungua kwa urahisi kisha kuirudisha mfukoni mwa mmoja kati ya walinzi hao wakati akiwa amelala fofofo.
Dr,kisinza amesema taarifa za kuibiwa kwa magari mawili majira ya alfajiri zinafuatia mmoja kati ya madereva alipokwenda kuchukua moja kati ya magari yaliyoibwa na kuwakuta walinzi wote wanne wakiwa wamelala fofofo na alipojaribu kuwaita hawakuitikia ndipo alipokwenda kwenye eneo magari yanapohifadhiwa na kubaini kuwa magari mawili likiwemo lile analoendesha aina ya ''land cruiser.
Hard top mkonga'' pamoja na lingine aina ya Land Cruiser GX hayapo huku lingine aina ya Toyota likiwa limevunjwa vioo baada ya jaribio lao la kutaka kuiba gari la tatu kushindikana.
Kufuatia hatua hiyo kamanda wa polisi mkoani Tanga bwana costantine massawe amesema jeshi la polisi limewatia mbaroni walinzi wote wanne kwa sababu wanashindwa kujieleza kuwa chakula walichokula wamepata wapi hatua ambayo inawapa mashaka kuwa huenda na wao wanahusika na tukio hilo.

