SEHEMU YA PILI
MAKAMU WA RAIS
Ibara ya 47.
Ibara ndogo ya (1),
Kutakuwa na Makamu wa Rais ambaye atakuwa ndiye Msaidizi Mkuu wa Rais kuhusu mambo yote ya Jamhuri ya Muungano kwa jumla, na hususan-
(a) atamsaidia Rais katika kufuatilia utekelezaji wa siku hata siku za Mambo ya Muungano;
(b) atafanya kazi zote atakazoagizwa na Rais;
(c) atafanya kazi zote za Rais kama Rais hayuko kazini au yuko nje ya nchi.
Ibara ndogo ya (2),
Bila ya kuathiri masharti ya ibara ya 37(5), Makamu wa Rais atapatikana kwa kuchaguliwa katika uchaguzi ule ule kwa pamoja na Rais, baada ya kupendekezwa na chama chake wakati ule ule anapopendekezwa mgombea kiti cha Rais na watapigiwa kura kwa pamoja. Mgombea kiti cha Rais akichaguliwa basi na Mahakmu wa Rais atakuwa amechaguliwa.
Ibara ndogo ya (3),
Mtu atateuliwa kugombea kiti cha Makamu wa Rais kwa kufuata kanuni kwamba endapo Rais wa Jamhuri ya Muungano atatoka sehemu moja ya Muungano, basi Makamu wa Rais atakuwa ni mtu anayetoka sehemu ya pili ya Muungano.
Ibara ndogo ya (4),
Mtu hatateuliwa kugombea au kushika kiti cha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano isipokuwa tu kama-
(a) ni raia wa kuzaliwa wa Jamhuri ya Muungano kwa mujibu wa sheria ya Uraia;
(b) ametimiza umri wa miaka arobaini;
(c) ni mwanachama na mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa;
(d) anazo sifa za kumwezesha kuwa Mbunge au Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi;
(e) katika kipindi cha miaka mitano kabla ya tarehe ya uchaguzi hajawahi kutiwa hatiani katika Mahakama yoyote kwa kosa lolote la kukwepa kulipa kodi yoyote ya Serikali.
Ibara ndogo ya (5),
Chama chochote hakitazuiwa kumpendekeza mtu yeyote kuwa mgombea kiti cha Makamu wa Rais kwa sababu tu kwamba mtu huyo kwa wakati huo ameshika kiti cha Rais wa Zanzibar au kiti cha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano.
Ibara ndogo ya (6),
Makamu wa Rais hatakuwa kwa wakati huo huo Mbunge, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano, wala Rais wa Zanzibar.
Ibara ndogo ya (7),
Endapo mtu ambaye ni Waziri Mkuu, au Rais wa Zanzibar anateuliwa au kuchaguliwa kuwa Makamu wa Rais ataacha kiti cha Waziri Mkuu, au cha Rais wa Zanzibar, kadri itakavyokuwa.
Ibara ndogo ya (8),
Makamu wa Rais atatekeleza madaraka yake chini ya uongozi na usimamizi wa Rais, na ataongoza na kuwajibika kwa Rais kuhusu mambo au shughuli zozote atakazokabidhiwa na Rais.
https://play.google.com/store/apps/details?id=tz.co.yetu.katiba.katiba