Rais Jakaya Mrisho Kikwete leo katika Ikulu ya Dar es Salaam amekabidhi vitabu 2,181 kwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa ajili ya vyuo vya Jeshi ili kuongeza taaluma.
Rais amekabidhi vitabu hivyo kwa Mkuu wa Majeshi Jenerali Davis Mwamunyange na kuahidi kuendelea kutafuta vitabu zaidi kwa ajili ya kuboresha Maktaba ya Jeshi iliyopo katika Chuo Cha Kijeshi kilichopo Monduli, Mkoani Arusha.
Library hiyo ilianzishwa na Mheshimiwa Rais wakati alipokuwa mkufunzi katika chuo hicho miaka iliyopita.
"Lazima mtenge bajeti kwa ajili ya vitabu lakini na mimi nitaendelea kutafuta vitabu niwaletee ili kuijengea uwezo Library yetu ya Monduli”.
Akipokea vitabu hivyo kwa niaba ya Jeshi, Jenerali Mwamunyange amemshukuru Rais kwa juhudi zake za kuboresha Jeshi la Wananchi Tanzania kwa ujumla na kulifanya kuwa la kisasa zaidi.
“Juhudi zako za kuliendeleza Jeshi letu imetuongezea uwezo na kujiamini zaidi. Bila juhudi zako tusingefika hapa tulipo na tunajivunia sana mafanikio haya” amesema Jenerali Mwamunyange .
Imetolewa na;
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,
Ikulu – Dar es Salaam.
28 Aprili,2014