Licha ya rekodi za Wizara ya Viwanda na Biashara kuonyesha kuwa asilimia 88 ya viwanda nchini ni vidogo zaidi, hakuna mkakati wowote wa kuvisaidia au kuvipatia ruzuku kama ambavyo vyama vya siasa vinapewa ruzuku ili vijiendeshe.
Wachumi wanashauri kuwa wakati umefika kwa Serikali kuangalia namna ya kuvisaidia viwanda vikiwamo vidogo ili viweze kuwa na nguvu ya kujiendesha.
Baadhi ya wakulima wanaamini kuwa kama Serikali ingewasaidia japo ruzuku kwa ajili ya kuanzisha viwanda vidogo au kuviboresha vilivyoko, Taifa lingeweza kuwa na maendeleo kwa kasi zaidi.
Wakulima DodomaWananchi wengi Dodoma wanalalamikia kukosekana kwa wateja katika mazao yao, hicho ni kilio ambacho pia kiko katika maeneo mengi nchini.
Katika jitihada za kukabiliana na tatizo la soko la zabibu linalowakabili wakulima wengi wa zao hilo, baadhi ya wakulima wameanzisha kiwanda kidogo cha kukamulia mchuzi (juisi) ya zabibu japo bado wanakabiliwa na changamoto nyingi.
Kiwanda hicho kidogo kinachoitwa Zawico Hombolo Company Ltd ambacho kiko katika Kijiji cha Hombolo Bwawani nje kidogo ya Manispaa ya Dodoma kilianzishwa na wakulima watatu ambao walikuwa wamechoshwa na ukosefu wa soko la zabibu zao kila msimu wa mavuno ya zabibu unapowadia.
Kwa kushirikiana kwa pamoja waliamua kuanzisha kiwanda hicho ambacho wangeweza kukitumia kwa kukamua mchuzi wa zabibu wanazolima na kisha kuuza mchuzi huo kwenye viwanda vikubwa vinavyotengeneza mvinyo.
Katibu wa Bodi ya Wakurugenzi wa kiwanda hicho, Rashid mkombozi, anasema nia ya kuanzisha kiwanda hicho ilikuwa njema japokuwa kwa sasa wanakabiliwa na changamoto kubwa ya mtaji wa kujiendesha.
Anasema awali wakati wanapata wazo la kuanzisha kiwanda hicho kidogo, walikuwa timu ya watu wanane. Lakini kutokana na kuchangia gharama mbalimbali wengi wao walijitenga na kubaki watatu.
Mweka Hazina wa kiwanda hicho, Emmanuel Chikwang’ala, anasema wamekuwa wakikumbana na changamoto nyingi zinazowafanye wasipate mafanikio waliyoyakusudia.