MKAZI wa mmoja wa Kijiji cha Igurubi Tarafa ya Igurubi Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kuwaingilia kimwili watoto wenye umri wa chini ya miaka kumi, baada ya kuwarubuni kwa kuwapa ubuyu na Sh 500 taslimu.
Hayo yamethibitishwa na Kamanda wa Polisi mkoani Tabora, Suzana Kaganda aliyesema tukio hilo ni la juzi katika Mtaa wa Muhaya Kijiji cha Igurubi. Alimtaja mtuhumiwa huyo kuwa ni Sudi Seif (47).
Alisema mtuhumiwa huyo anadaiwa kuwatendea unyama watoto hao, kwa kuwalaghai kuwapa ubuyu na pesa, endapo wangemkubalia kufanya tendo la mapenzi.
Alisema kwa kuwa watoto hao walikuwa wadogo, alifanikiwa kuwashawishi, na alianza kwa kumchukua mtoto wa kwanza mwenye umri wa miaka 5 na miezi 4, anayesoma chekechea Shule ya Msingi Igurubi.
Kamanda huyo aliongeza kuwa, akiwa chumbani na mtoto huyo alimwingilia kimwili katika sehemu zote za siri na kumsababishia maumivu makali hadi wazazi wake walipomgundua wakati aliporudi nyumbani muda wa jioni.
Alidai kuwa baada ya tukio hilo kwa mtoto wa kwanza, alimchukua mtoto mwingine mwenye umri wa miaka 9 anayesoma darasa la pili Shule ya Msingi Ikonda Kata ya Igurubi, aliyemfanyia kama mtoto wa kwanza.
Kaganda alisema baada ya matukio hayo, mtuhumiwa aliendelea kujipumzisha nyumbani kwake, lakini ghafla alivamiwa na kundi la wanakijiji waliopanga kumdhuru.
Hata hivyo, mtu huyo aliokolewa na askari wa Kituo kidogo cha Polisi Igurubi, waliomchukua na kumpeleka Kituo kikuu cha Polisi mjini Igunga.
Kaimu Muuguzi Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Igunga, Mashaka Hilaly alithibitisha kuingiliwa kimwili kwa watoto hao na kusema wameharibiwa vibaya katika sehemu zote za siri, hali iliyolazimu kuwalaza hospitalini.
Jiunge na mi kwa kubonyeza kwenye link zifuatazo chini ili kupata habari mpya zaidi.
FACEBOOK >>> TWITTER >>> MATUKIO KWA NJIA YA SAUTI