Wengi tumekuwa tukitumia mdalasini kama mojawapo ya kiungo kinachosaidia kuweka harufu nzuri kwenye chai na chakula. Harufu ya kiungo hiki pia mara nyingi imekuwa ikisikika kwenye pilau.
Kutokana na uelewa huo wengi tumekuwa tukiishia kutumia mdalasini kama kiungo bila kufahamu kuwa kuna faida kadhaa za kiafya tunazoweza kuzipata kupitia mti huu.
Licha ya kusaidia kwa kiasi kikubwa katika kuzuia kusambaa kwa ugonjwa wa saratani mwilini mti huu unatajwa kuwa kinga ya asili ya meno na fizi.
Usichokijua ni kwamba mdalasini una virutubisho ambavyo hufanya kazi ya kulinda kinywa na kuondoa uwezekano wa kushambuliwa na bakteria.
Mtandao wa Sunwarrior unabainisha kuwa uwapo wa mdalasini kwenye chai unasaidia kinywa cha mnywaji kuwa na meno na fizi zenye afya.
Sambamba na tiba hiyo mdalasini ni dawa nzuri kwa watu wenye tatizo la kunuka mdomo kwani husaidia kukata harufu.