Watu watano wasiofahamika wanaodhaniwa ni wezi, wamemvamia dereva wa lori la mafuta, Stephano John eneo la Kibamba, Barabara Kuu ya Dar es Salaam -Morogoro alipokuwa katika foleni na kisha kumpiga, kumjeruhi sehemu kadhaa za mwili, kumfunga kamba na kumtupa mtaroni.
Ilielezwa kuwa baada ya kumfunga kamba, wahalifu hao walimdhibiti ndani ya lori na kutembea naye umbali wa kilomita moja walipofika maeneo ya Kiluvya ambako walimtupa katika mtaro na kuendelea na safari. Walifika mizani Kibaha wakapima uzito wa gari kama kawaida na kutokomea.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei alisema tukio hilo lilitokea saa mbili usiku wakati dereva huyo akiwa kwenye foleni na lori lake aina ya Scania lililokuwa na tela pia lilikuwa na shehena ya petroli lita zaidi ya 39,000.
“Wakati dereva akiwa katika mwendo wa polepole kwenye foleni ya malori kuingia mizani, alivamiwa ghafla na watu watano waliofungua mlango na kuingia ndani.
“Wakati dereva akishangaa, walimnyanyua kwenye kiti na kumweka kiti cha nyuma na wakimtaka kukaa kimya,” alisema.
Kamanda Matei alimkariri dereva huyo akisema watu watatu walikaa kiti cha nyuma na mmoja kiti cha mbele na mwingine alikaa cha dereva na kuendesha lori hilo na yeye akiwa amewekwa chini ya ulinzi.
“Usiku wa manane wasamaria wema walimkuta dereva huyo akiwa ameumizwa na akiwa amefungwa na walimpa msaada wa kumfungua kamba kisha kumfikisha Kituo cha Polisi Maili Moja, lakini walimwambia anatakiwa kutoa maelezo Kituo cha Polisi Tumbi. Lakini baada ya kutoa maelezo yale, ndipo msako ulipoanza kwa kushirikiana na mikoa jirani.”
Akizungumza baadaye jana, Ofisa Habari wa Polisi Mkoa wa Pwani, Hassan Jumanne alisema katika msako uliofanyika juzi, lori hilo lilipatikana likiwa limetelekezwa eneo la Lugoba likiwa limeibwa mafuta yaliyokuwa katika tanki la tela.
Jumanne alisema uchunguzi wa awali ulibaini kuwa lita za mafuta zilizoibwa ni 5,450 yenye thamani ya Sh11 milioni na kusema msako wa kuwatafuta waliohusika na tukio hilo unaendelea.
Awali, dereva Stephano alisema alikuwa akielekea Karatu na alifikwa na mkasa huo wakati utingo wake akiwa ametangulia mizani na kufanya ununuzi wa vyakula vya njiani ili kuokoa muda.
Hata hivyo, alisema utingo huyo alipoliona lori hilo mizani na kulifuata tayari kuendelea na safari, watu hao walimzuia.