Baada ya kusubiri kwa miezi tisa, siku imefika na mtoto aliyekuwa akitarajiwa kwa hamu anakaribia kuzaliwa. Kwa muda mrefu, mlango wa tumbo la uzazi la mama mjamzito umefungwa kabisa ili kumlinda mtoto aliye tumboni. Lakini sasa misuli ya mlango huo inalegea na kufunguka. Muujiza wa kuzaa unaanza.
Ni nini huchochea hatua ya kujifungua? Kuna mambo mengi yanayohusika, lakini mawili ni yenye kustaajabisha. Kwanza homoni inayoitwaoxytocin ambayo hutengenezwa katika ubongo hutokezwa. Watu wote, wanaume na wanawake hutokeza homoni hiyo, lakini mama mjamzito huitokeza kwa wingi uchungu wa kuzaa unapoanza, na hivyo kufanya mlango wa tumbo la uzazi ufunguke na misuli ya tumbo la uzazi ikazike.Haijulikani jinsi tezi pituitari ya mama mja-mzito inavyojua wakati wa kutokeza homoni hiyo.
Kitabu Incredible Voyage—Exploring the HumanBody kinasema hivi: “Kwa njia fulani, ubongo wake unajua kwamba kipindi cha ujauzito kimekamilika na kwamba ni wakati wa misuli yenye nguvu ya tumbo la uzazi . . . kuanza kazi yake muhimu.”Jambo la pili katika hatua hii ni kazi ya kondo la nyuma ambalo huzuia kutokezwa kwa homoni ya projesteroni. Wakati wa ujauzito, projesteroni huzuia mikazo mikali ya tumbo la uzazi. Lakini sasa kwa kuwa homoni hiyo haitokezwi, tumbo la uzazi huanza kukazika.
Kwa kawaida, uchungu wa kuzaa huchukua kati ya saa 8 hadi 13, kisha mtoto anasukumwa hadi kwenye mlango wa tumbo la uzazi uliolegea na kufunguka. Baadaye, kondo la nyuma hutoka.Kitoto hicho kichanga lazima kizoee haraka mazingira yake mapya ambayo ni tofauti sana na tumbo la uzazi mama. Kwa mfano, akiwa ndani ya tumbo la uzazi, mapafu ya mtoto yalikuwa yamejaa maji yanayomzunguka mtoto tumboni, ambayo hutoka anapopita kwenye njia ya uzazi.
Sasa lazima mapafu yajazwe hewa ili aanze kupumua, na hilo hutukia mtoto anapolia kwa mara ya kwanza. Mabadiliko ya haraka hufanyika pia moyoni na katika mfumo wote wa kuzungusha damu. Shimo fulani linalounganisha vyumba viwili vya juu vya moyo na mshipa wa damu unaopitisha damu hadi kwenye mapafu hujifunga, ili damu izunguke kwenye mapafu, na hivyo damu hufyonza oksijeni. Inashangaza kwamba mabadiliko hayo nje ya tumbo la uzazi hufanyika haraka sana.Hatua yote ya kuanza kwa uchungu wa kuzaa hadi mtu anapojifungua inatukumbusha maneno haya ya Biblia:
“Kuna wakati uliowekwa wa kila kitu, hata kuna wakati wa kila jambo chini ya mbingu.” Huo unatia ndani “wakati wa kuzaliwa.” (Mhubiri 3:1, 2) Bila shaka utakubali kwamba mabadiliko ya homoni na ya kimwili ambayo hutukia kwa saa chache tu, ni uthibitisho wa ubuni wa Muumba wetu, ambaye Biblia inasema ndiye “chemchemi ya uzima.”—Zaburi 36:9; Mhubiri 11:5.