Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), liliundwa rasmi Septemba Mosi, 1964. Ni Jeshi lililosaidia nchi nyingi za Kusini mwa Bara la Afrika kupata uhuru wake hasa zile zilizokuwa bado zinatawaliwa.
Tangu Jeshi hili liundwe, limetekeleza majukumu yake ya msingi kwa mafanikio makubwa kutokana na ushirikiano mzuri baina yake na wananchi na wadau mbalimbali.
Majukumu ya JWTZ ni pamoja na kulinda Uhuru wa nchi, Mipaka, Watu na mali zao.
Pili, Kusaidia mamlaka za kiraia katika usalama na dharura mbalimbali kama maafa na majanga. Aidha pamoja na majukumu hayo JWTZ limekuwa likitoa misaada ya huduma za kijamii kwa wananchi, na vile vile linashiriki katika operesheni za Ulinzi wa Amani Duniani chini ya Umoja wa Mataifa, na Umoja wa Afrika. Kutokana na mafanikio hayo, nchi yetu imeendelea kuwa kisiwa cha usalama, amani na utulivu.
Hali hiyo imewafanya wananchi kuendelea na majukumu yao ya uzalishaji mali bila wasiwasi wala hofu.
Amani na utulivu huo, pia vimekuwa kivutio kikubwa kwa mataifa mbalimbali kushirikiana na nchi yetu. Hali hiyo inawapa fursa nzuri na ya uhakika wawekezaji kuja kuwekeza katika miradi mbalimbali hapa nchini.
Miradi hiyo inasaidia kuwapatia ajira wananchi na wakati huo inachangia kuinua uchumi wa Taifa letu.
Kufuatia mafanikio hayo, natoa pongezi za dhati kwa wanajeshi wote wa ngazi na fani mbalimbali kwa kutekeleza majukumu yao kwa bidii, utii, uhodari, nidhamu, uadilifu na weledi, hivyo kudumisha Amani na Utulivu endelevu nchini.
Naishukuru Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jitihada zake mbalimbali za kuendelea kulijengea uwezo Jeshi letu kwa kulipatia fedha, zana na vifaa vya kisasa pamoja na makazi bora katika kutekeleza dhana ya nchi yetu kuwa na Jeshi dogo lenye wataalam na lililotayari wakati wote.
Shukrani za dhati nazielekeza pia kwa wananchi na wadau mbalimbali kwa kushirikiana vyema na Jeshi lao katika kuliwezesha kutekeleza majukumu yake ipasavyo. Ushirikiano huo ni muhimu uendelee kudumishwa wakati wote.
JWTZ litaendelea kutekeleza wajibu wake na kushirikiana kwa karibu na Vyombo vingine vya Usalama pamoja na Umma wa Watanzania kwa ujumla katika kudumisha amani na utulivu uliodumu kwa miaka mingi hapa nchini bila kutetereka.
Mungu Ibariki JWTZ, Mungu Ibariki Tanzania.