MKALI anayetamba na nyimbo ‘Sugua Gaga’ na ‘Lava Lava’, Sarah Kaisi ‘Shaa’, amekana taarifa zinazoenea kwamba ana ujauzito.
Katika mazungumzo yake na Mwanaspoti, Shaa alikiri kuweka picha zilizoonyesha nguo za watoto kwenye mtandao wa Instagram sambamba na kuandika ujumbe ‘shopping ya mtoto imeanza’ .
“Ni kweli niliweka picha ya nguo za mtoto zikiwa dukani wakati nikichagua nguo za kununua kwa ajili ya mtoto wa rafiki yangu,” alisema.
“Lakini ile haina maana kwamba ninatarajia kupata mtoto, unapoandika kitu haina maana kwamba umesimama katika hilo inaweza kuwa kwa upande mwingine pia. Ni kama ilivyokuwa katika suala la picha hiyo.
”
Hata hivyo katika mazungumzo yake na Mwanaspoti katika siku za karibuni, mwanamuziki huyo aliweka wazi kwamba angependa kupata watoto wawili siku za usoni.
Picha hiyo aliyoweka mtandaoni imezua gumzo kubwa kwa mashabiki wake ambao inaonekana wazi jinsi wanavyosubiri kwa hamu kumuona mwanamuziki huyo akiwa amebeba ujauzito.